Oct 18, 2020 14:53 UTC
  • Afisa mkuu wa zamani wa White House: Wamarekani tafakarini sana kabla ya kupiga kura ya urais

Mkuu wa zamani wa ofisi ya wafanyakazi wa Ikulu ya rais wa Marekani ya White House amesema, rais wa nchi hiyo Donald Trump ni mtu kigeugeu na akashauri kwamba, wapigakura wa Marekani watafakari sana kabla ya kumchagua rais wao ajaye.

Kwa mujibu wa televisheni ya CNN, John Kelly amemtaja Rais Donald Trump wa Marekani kama "mtu mwenye dosari kubwa zaidi za kitabia aliyewahi kumwona maishani mwake".

Kelly, ambaye alihudumu kwa muda wa miaka miwili katika serikali ya Trump akiwa Waziri wa Usalama wa Ndani na Mkuu wa Ofisi ya Wafanyakazi wa Ikulu ya White House amebainisha kuwa, "Kiwango cha udanganyifu na hulka ya ulaghai ya Trump katika namna anavyoamiliana na watu vinasikitisha sana."

Tangu Januari 2019 na baada ya kushtadi tofauti na mivutano kati yake na Trump, John Kelly, ambaye pia ni jenerali mstaafu wa jeshi la wanamaaji la Marekani alijiuzulu wadhifa wake kama Mkuu wa Ofisi ya Wafanyakazi wa Ikulu ya rais na nafasi yake ikachukuliwa na Mick Mulvaney.

John Kelly

Sera zinazogongana, tabia chafu za ufuska, uchukuaji hatua zisizotabirika na uendeshaji mbovu wa mambo vimeporomosha sana kiwango cha uungaji mkono wa Wamarekani kwa Trump.

Uchaguzi wa rais wa Marekani utafanyika Novemba 3 ambapo Trump atachuana na mgombea wa chama cha Democrat, Joe Biden ambaye hadi sasa, ndiye anayeonekana kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda uchaguzi huo.../

Tags