Oct 19, 2020 02:30 UTC
  • Kukiri mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani malengo halisi ya Washington dhidi ya Iran

Tarehe 8 Mei 2018 Marekani chini ya utawala wa Donald Trump, ilijitoa kwenye mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA na kuiwekea Iran vikwazo vikubwa zaidi ambavyo havijawahi kutokea. Ijapokuwa awali serikali ya Trump ilidai kuwa inataka mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaangaliwe upya ndio maana imejitoa kwenye makubaliano hayo, lakini hivi sasa inatangaza waziwazi lengo lake hasa la kujitoa kwenye mapatano hayo.

Robert O'Brien, mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani, siku ya Ijumaa alisema katika mkutano uliofanyika kwa njia ya video kwamba iwapo Trump atashinda katika uchaguzi ujao, basi Marekani itaiwekea vikwazo vya kiuchumi Iran kiasi kwamba Tehran italazimika kusalimu amri na kukubali kufanya mazungumzo kwa nguvu na Marekani ambayo yatafuta kabisa miradi ya nyuklia ya Tehran. Alikiri pia kwamba, kujitoa Marekani kwenye mapatano hayo na kuiwekea vikwazo vikubwa mno Tehran si tu hakujaizuia Iran kuendelea na mradi wake wa nyuklia, lakini pia shughuli zake hizo zimeongezeka na kuwa nyingi zaidi.

Kwa kweli inachotaka Marekani ni kuiona Iran inaachana na uwezo na elimu yake yote iliyo nayo kuhusu teknolojia ya nyuklia, na kama italazimu kuwa na teknolojia hiyo, basi iwe ya kugaiwa, na ya kuendeshwa na kusimamiwa kikamilifu na madola ya kigeni. O'Brien amesema, tunaweza kukubali Iran kuwa na mradi wa nyuklia lakini mradi huo usiwe kama wa hivi sasa ambao unategemea wataalamu wake wa ndani ambao taasisi zake ziko chini ya ardhi na ambazo wananchi wa Iran wanaweza kuziendeleza wakati wowote wanaotaka. 

Robert O'Brien, mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani

 

Mshauri huyo wa usalama wa taifa wa Marekani ameshindwa kuficha hamaki zake kwa kuona taifa la Iran limefanikiwa kuwa na teknolojia inayojitegemea ya nyuklia. Ameonesha wazi kuwa, anachukizwa mno kuona Iran inaweza kustawisha uchumi wake kwa teknolojia ya nyuklia katika nyuga tofauti kama za uzalishaji umeme, viwanda, katika masuala ya afya na tiba, kilimo n.k. Ndoto ya viongozi hao wenye chuki isiyomithilika wa Marekani, ni kuiona Iran inaachana na manufaa yote hayo ya nishati ya nyuklia na badala yake inakubali teknolojia ya kugaiwa, ndogo, na ya kuendeshwa na kusimamiwa na watu baki.

Suala jingine lililosemwa waziwazi na mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani katika mkutano huo uliofanyika kwa njia ya Intaneti, ni kushikilia kwake kwamba Iran isiwe na nguvu zozote za kiulinzi na iachane na uwezo wake wa makombora. Afisa huyo mwandamizi wa Marekani amegusia mradi wa makombora wa Iran na kudai kuwa nguvu hizo ni tishio kwa Ulaya na Marekani. Amesema: Mradi wa makombor wa wa Iran ni tishio kwa usalana na Marekani na inabidi Iran ipokonywe nguvu hizo kwenye meza ya mazungumzo. Madai hayo yanatolewa na nchi kama Marekani ambayo ndiyo isiyoaminika zaidi kuwa na silaha kama hizo. Marekani ndiyo nchi pekee duniani yenye historia ya kutumia mabomu ya atomiki kuangamiza raia. Historia yote ya Marekani imejaa jinai za kivita, uvamizi na ubeberu dhidi ya mataifa mengine. Wakati Iran kwanza imethibitishwa kimataifa kuwa mradi wake wa nyuklia ni wa amani kikamilifu, si wa silaha za nyuklia. Pia haina historia ya kuvamia nchi yoyote, tofauti na Marekani na madola mengine ya kibeberu. 

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo

Jambo jingine lililomkasirisha mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani na kushindwa kuficha hamaki zake, ni ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili na kuwa kwake kikwazo kikubwa cha siasa za kibeberu za Marekani katika eneo la Asia Magharibi. O'Brien amehamakishwa mno na uungaji mkno wa Iran kwa harakati za ukombozi za eneo hili kama vile Hizbullah ya Lebanon, HAMAS ya Palestina na Answarullah ya Yemen. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, matamshi hayo ya O'Brien si mapya, bali ni kukariri yale yale masharti 12 yaliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo mwezi Mei 2008 wakati Trump alipotangaza kuitoa Washington katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA.

Hata hivyo, taifa la Iran limekabiliana na vikwazo vya kiwango cha juu vya Marekani kwa muqawama wa kiwango cha juu na kufelisha njama za Trump na genge lake huko White House. Mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Marekani, Paul Pillar amesema: Hatua za serikali ya Marekani za kuongeza vikwazo kwa ajili ya kuipigisha magoti Iran, zimefeli.

Tags