Oct 19, 2020 08:03 UTC
  • Russia yaitaka Marekani isitishe kauli za kichochezi dhidi ya Iran

Mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Russia amemtaka Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo kuacha tabia yake ya kutoa kauli za kichochezi dhidi ya Iran.

Dmitry Polyanskiy, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema Pompeo pia anapaswa kusitisha sera za kumimina silaha katika eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) iwapo anataka amani iwepo katika eneo. Aidha amemtaka aache kutumia misamiati kama vikwazo na adhabu na badala yake atumie maneno kama vile mazungumzo ili Marekani iweze kuheshmiwa tena.

Polyanskiy ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter ambapo amemnukulu Pomepo akitoa vitisho kwa wale ambao watafanya biashara ya silaha na Iran. Pompeo amedai kuwa biashara ya silaha na Iran itakiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Mike Pompeo

Kauli hiyo ya Pompeo imekuja baada ya vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kufika ukingoni. Baada ya kupita miaka mitano ya utekelezaji wa mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA, hatimaye muda wa vikwazo vya silaha vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulimalizika jana Jumapili, Oktoba 18, 2020. Sasa Iran iko huru kisheria kuuza na kununua silaha na zana za kivita nje ya nchi. Aidha vikwazo vya kusafiri nje maafisa 23 wa kisheria wa Iran vimeondolewa kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha makubaliano ya JCPOA.