Oct 20, 2020 02:29 UTC
  • Waislamu wafukuzwa Ufaransa kwa kisingizio cha kupambana na misimamo mikali

Mwenendo wa kuenezwa chuki na kejeli dhidi ya itikadi za Kiislamu umekuwa ukiongezeka kwa kasi kubwa nchini Ufaransa katika miaka ya karibuni.

Wakati huo huo ubaguzi na mashinikizo yamekuwa yakiongezeka dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo kwa visingizio mbalimbali vikiwemo eti vya kupambana na ugaidi na misimamo ya kupindukia.

Katika hatua ya hivi karibuni katika uwanja huo, serikali ya Ufaransa imekusudia kuwafukuza Waislamu wapatao 231 wanaoishi nchini humo kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya kupindukia mpaka. Serikali ya Paris imechukua hatua hiyo kufuatia tukio la hivi karibuni la kuuliwa mwalimu mmoja wa historia wa nchi hiyo na raia wa Chechnia.

Kwa kutilia maanani kwamba Ufaransa ndiyo nchi iliyo na idadi kubwa zaidi ya jamii ya Waislamu barani Ulaya, ni wazi kuwa imekuwa ikishuhudia wimbi kubwa la hujuma na vitendo vya chuki na udhalilishaji dhidi ya Uislamu kwa lengo la kuharibu jina zuri la Uislamu na Mtume Mtukufu (saw), jambo ambalo bila shaka limepata jibu kutoka kwa Waislamu wa nchi hiyo.

Mfano wa chuki hiyo inayoenezwa katika nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu ni kitendo kilichofanywa na mwalimu huyo aliyeuawa kwa jina la Samuel Paty cha kuwaonyesha tena wanafunzi wake vikatuni vinavyomdhalilisha Mtume Mtukufu (saw) vilivyochapishwa na jarida la Charlie Hebdo la huko huko Ufaransa.

Emmanuel Macron wa Ufaransa, mwenye chuki kali dhidi ya Uislamu

Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo amekitaja kitendo cha kuuawa mwalimu huyo kuwa ni shambulio la 'ugaidi wa Kiislamu' ambalo limetelekezwa dhidi ya mwalimu wa miaka 47 ambaye alikuwa anawafunza wanafunzi wake eti somo la 'uhuru wa kujieleza.'

Rais huyo amekitambua kitendo cha kutusi na kuudhalilishwa Uislamu kuwa ni 'uhuru wa kijieleza' katika hali ambayo nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za Magharibi ambazo zinachukulia  kitendo cha kupinga madai ya kutokea mauaji ya holocaust dhidi ya Mayahudi, kuwa hatia kubwa.

Macron anatumia kisingizio cha 'uhuru wa kusema' kuhalalisha kitendo cha jarida la Charlie Hebdo cha kudhalilisha matukufu ya Uislamu katika hali ambayo kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maana halisi ya 'uhuru wa kujieleza', hakuna mtu anayeruhusiwa kutusi wala kukosea heshima itikadi za kidini za watu wengine.

Badala ya rais huyo na serikali yake kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kupunguza vitendo vya wanaoneza chuki dhidi ya Uislamu na matukufu ya Uislamu na hasa kuhusu Mtume Mtukufu (saw), ameamua kuchochea zaidi wanaoeneza chuki hiyo, na hivyo kuamsha hasira ya Waislamu, ambapo baadhi wameamua kujibu mapigo kwa njia tofauti, kikiwemo kitendo cha hivi karibuni katika mojawapo ya viunga vya Paris.

Kwa kufukuza baadhi ya Waislamu wanaoishi huko Ufaransa, serikali ya Macron inajaribu kujivua uwajibikaji katika uwanja huo na kuonyesha kuwa haihusiki kivyo vyote na kuchochea hisia zilizo dhidi ya Uislamu na pia kulea ugaidi wa kitakfiri nchini humo. Hii ni katika hali ambayo nchi hiyo ikishirikiana na nchi nyingine za Ulaya na kwa uchochezi wa Marekani, imekuwa na nafasi muhimu katika kueneza vitendo vya mabavu na ugaidi wa makundi ya kigaidi kama Daesh katika eneo la Asia Magharibi.

Magaidi wa Daesh walioanzishwa na nchi za Magharibi kuvuruga Uislamu

Frédéric Poisson, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi anasema: Marekani na Ufaransa zimeshirikiana kwa karibu katika kuanzisha kundi la Daesh.

Lengo la nchi za Magharibi la kuanzisha kundi hilo la kigaidi lilikuwa ni kuiangusha serikali halali ya Syria na hatimaye kusambaratisha mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika eneo, ambapo Syria ina nafasi muhimu katika mapambano hayo. Pamoja na hayo, kundi hilo katika maiaka ya karibuni limewageukia mabwana zake hao wa Magharibi, ambapo limetekeleza mashambulio kadhaa ya kigaidi nchini Ufaransa.

Nchi hiyo badala ya kukubali makosa yake katika uwanja huo, imekuwa ikichukua hatua za kimaonyesho tu kama vile kuwafukuza watuhumiwa wa vitendo hivyo nchini humo ili kujaribu kupunguza mashambulio ya magaidi katika ardhi yake. Nchi hiyo ilipanda yenyewe mbegu hiyo ya ugaidi na sasa inapasa kuvuna mazao yake bila klalamika.

Wakati huo huo serikali ya Paris inapasa kufanya juhudi za kuzuia kutokea kitendo kingine kama cha hivi karibuni katika kiunga cha mji huo, kwa kuzuia chuki na udhalilishaji dhidi ya Uislamu, na hasa kuvunjiwa heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw).

Tags

Maoni