Oct 20, 2020 02:35 UTC
  • Wafuasi na wapinzani wa Trump wapambana vikali katika mji wa Boston

Maafisa wa jimbo la Massachusetts nchini Marekani wamesema, kumetokea mapigano kati ya waungaji mkono na wapinzani wa rais Donald Trump katika jimbo hilo.

Kwa mujibu wa maafisa hao, wafuasi na waungaji mkono wa Trump walipambana kwenye uwanja wa Copley katika maandamano yaliyofanyika jana Jumatatu.

Katika maandamano hayo, wapinzani wa rais wa Marekani walizichoma moto kofia za kampeni za kiongozi huyo zenye maandishi ya kaulimbiu "Tuirejeshee Marekani hadhi yake" pamoja na nembo zingine za kumuunga mkono. Badala yake walibeba mabango yaliyoandikwa "Trump lazima aondoke".

Wapinzani wa Trump wakibeba mabango yenye maandishi ya kumpiga vita  

Mkabala na wapinzani wa Trump, waungaji mkono wake walibeba mabango yenye kaulimbiu za kuipiga vita China pamoja na bendera za kampeni za kiongozi huyo.

Maandamano hayo na mapigano baina ya wafuasi wa Trump na Wamarekani wanaompinga yamejiri zikiwa zimesalia takribani wiki mbili tu kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani utakaofanyika tarehe 3 ya mwezi ujao wa Novemba.

Trump amekuwa akiunga mkono kila mara vitendo vya fujo na utumiaji nguvu vinavyofanywa na wafuasi na waungaji mkono wake wakuu, ambayo ni makundi ya wazungu wanaojiona bora kuliko watu wa asili nyingine, kwa ajili ya kushambulia maandamano ya wananchi wanaompinga.

Matokeo ya chunguzi nyingi za maoni zilizofanywa hivi karibuni yanaonyesha kuwa mshindani mkuu wa Trump, Joe Biden anayegombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic ana nafasi kubwa zaidi ya kushinda uchaguzi huo.../

 

Tags