Oct 20, 2020 07:59 UTC
  • Russia yaitaka Marekani iache kujifanya 'polisi wa dunia'

Russia imeikosoa vikali Marekani kwa kufuata tena mkondo ghalati wa kuzishinikiza nchi za dunia zifuate sera, matakwa na maagizo yake.

Dmitry Polyanskiy, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema hayo katika ujumbe wa Twitter ambapo amekosoa hatua ya Marekani ya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya kampuni za China kwa kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema: Hatua yenye makosa tena...Marekani kujifanya polisi wa dunia, na kuchukua nafasi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni jambo lisilokubalika. 

Ameongeza kuwa, Moscow inafanya na itaendelea kufanya biashara na Tehran; na Marekani haina haki ya kuiambia Russia au nchi yoyote cha kufanya au kutofanya. Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Russia amewataka watawala wa Washington waache kuidhalilisha Marekani na kuiweka nchi hiyo katika mkondo ambao hauelekei popote.

Matamshi haya ya Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa yamekuja baada ya Marekani kuwawekea vikwazo raia wawili wa China na taasisi sita za Kichina, kwa kufanya muamala wa kibiashara na Shirika la Usafirishaji Bidhaa Baharini la Iran (IRISL).

Shehena za Shirika la Usafirishaji Bidhaa Baharini la Iran (IRISL) bandarini

Hii ni katika hali ambayo, baada ya kupita miaka mitano ya utekelezaji wa mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA, hatimaye muda wa vikwazo vya silaha vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulimalizika Jumapili, Oktoba 18, 2020. 

Sasa Iran iko huru kisheria kuuza na kununua silaha na zana za kivita nje ya nchi. Aidha vikwazo vya kusafiri nje maafisa 23 wa kisheria wa Iran vimeondolewa kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha makubaliano ya JCPOA. 

Tags

Maoni