Oct 20, 2020 11:04 UTC
  • Kupitishwa sheria mpya ya usafirishaji bidhaa nyeti za China kwa ajili ya kukabiliana na Marekani

Duru rasmi za habari nchini China zimeripoti habari ya kupasishwa sheria mpya ambayo inadhibiti usafirishwaji nje ya nchi bidhaa za nchi hiyo lengo likiwa kukabiliana na Beijing na mataifa ambayo yamechukua hatua za kudhibiti maslahi ya nchi hiyo.

Sheria hiyo ambayo inajumuisha mashirika yote ya China ilipasishwa Jumapili iliyopita na kamati ya kudumu ya Bunge la China (Kongresi ya Kitaifa ya Jamhuri ya Watu wa China) itaanza kutekelezwa tarehe Mosi Desemba mwaka huu. Kwa mujibu wa duru za habari za China, sheria hiyo mpya inatoa ruhusa ya kuchukua hatua mkabala za ulipizaji kisasi za Marekani.

Kupasishwa sheria mpya inayotoa mwongozo wa bidhaa za China zinazosafirishwa nje ya nchi kunajiri katika hali ambayo, katika miezi ya hivi karibuni Marekani imechukua hatua mara kadhaa ikifanya juhudi za kupiga marufuku shughuli za mashirika kama ya teknolojia ya China ambayo yanatoa huduma za kudhamini vifaa vya mawasiliano, upashaji habari na ufikishaji ujumbe nchini Marekani kwa kile ilichosema, kuwa tishio shughuli za mashirika hayo kwa usalama wa taifa wa Washington. Hatua hizo za Marekani zimelenga kufunga milango ya kuingia katika soko la nchi hiyo bidhaa hizo za China na hata katika nchi nyingine.

 

Hata hivyo mzozo na mvutano wa China na Marekani haujaishia katika mambo hayo tu, kwani ni kwa muda sasa Beijing na Marekani zimekuwa zikivutana mashati kuhusiana na masuala mbalimbali kama ya biashara, haki za binadamu, teknolojia na hata kadhia ya virusi vya Corona. Mivutano hiyo imepelekea kuibuka hiitilafu za kimsingi baina ya mataifa hayo mawili makubwa. Hivi sasa swali la kimsingi linaloulizwa na weledi wa mambo ni kuwa, kwa nini katika miezi ya hivi karibuni, Rais Donald Trump wa Marekani ameshadidisha mashinikizo yake dhidi ya China?

Akthari ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, Trump amechukua hatua hizo za kichochezi ili kujipigia debe na kujiongezea karata katika uchaguzi wa mwezi ujao na hivyo kujiandalia mazingira ya kuibuka na ushindi. Kwa maneno mengine ni kuwa, kutokana na kukaribia kufanyika uchaguzi nchini Marekani, Trump ameongeza mashinikizo yake dhidi ya China akiwa na lengo la kuwavutia wapiga kura ili wamchague kwani anajionyesha kuwa yeye ndiye mwokozi wa tabaka la wafanyakazi nchini Marekani. Kwa kutumia mbinu hiyo hiyo, Trump amekuwa akiwashinikiza waitifake wake wakongwe ili waungane naye katika vita vya kiuchumi dhidi ya China.

Hata hivyo kile ambacho kiko wazi ni kuwa, juhudi za Trump za kushadidisha mashinikizo dhidi ya China katika siku hizi za kampeni za uchaguzi za lala salama, mbali na kuwa hazijawa na taathira yoyote kwa sera za Beijing katika eneo, bali kutokuwa na imani na ahadi za Trump kumewafanya waitifaki wa Washington kusini mashariki mwa Asia kutomuunga mkono Trump katika vuta nikuvute baina yake na China.

 

Kwa maneno mengine ni kuwa, kwa kuzingatia maendeleo mwafaka iliyoyapata China, imeweza siku zote kuyavutia mataifa mengine kupitia mapendekezo yake hayo; na jambo hilo linashuhudiwa kwa uwazi zaidi katika eneo la kusini mashariki mwa Asia.

Hata hivyo, China nayo haijakaa bure na kuyakodolea macho tu mashinikizo ya Marekani, bali imechukua hatua mkabala na hizo na ikiwa na lengo la kutunisha misuli na kuonyesha nguvu zake katika eneo la kusini mashariki mwa Asia haijasita kuchukua hatua yoyote ile. Kuongeza manuva yake ya kijeshi katika eneo hilo, kuiwekea mashinikizo Taiwan na kutekeleza sheria mpya ya usalama wa taifa huko Hong Kong baada ya machafuko ya hivi karibuni ambapo Marekani ilikuwa mmoja wa wahusika wakuu, ni miongoni mwa hatua ambazo Beijing imechukua kwa minajili ya kukabiliana na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya mashariki mwa Asia na masuala ya ndani ya China.

Vita vya kibiashara kati ya Cina na Marekani

 

Vyovyote itakavyokuwa, kupasishwa na Beijing sheria mpya ya usafirishaji nje ya nchi bidhaa nyeti ambayo itaanza kutekelezwa Disemba Mosi mwaka huu, kunajiri katika hali ambayo, katika miezi ya hivi karibuni, Marekani imechukua hatua kali dhidi ya shughuli za mashirika ya teknolojia ya China kama Huawei jambo ambalo liliikasirisha mno China.

Tukiachana na mtazamo wa kiuchaguzi wa Trump kwa ajili ya kukabiliana na China, wajuzi wengi wa mambo wanaamini kuwa, China ikitumia njia ya amani imeingia katika ulingo wa mashindano na Marekani, ushindani ambao umekuwa ukishika kasi siku baada ya siku. Serikali ya Marekanii imekuwa ikitekeleza siasa za kuiondoa China katika ulingo wa ushindani ikitumia nyenzo za kieneo na kimataifa. Kimsingi ni kuwa, majimui ya siasa za Marekani kuanzia vita vya kibishara mpaka kuiuzia silaha Taiwan, yote hayo yanafanyika katika fremu ya kuifuta China. Hata hivyo, utendaji wa Trump usio wa kidiplomasia pamoja na wasiwasi wa viongozi wa ukanda wa kusini mashariki mwa Asia wa kutoheshimu ahadi zake Rais huyo wa Marekani, ni anga ambayo imeifanya hali ya mambo kuondoka katika utuvuli na kufanya mizani iinamie upande wa China.

Maoni