Oct 21, 2020 02:36 UTC
  • Ahadi ya Marekani; kuondolewa jina la Sudan katika orodha ya mataifa yanayounga mkono ugaidi

Majadiliano baina ya Marekani na Sudan yangali yanaendelea huku kila upande ukijaribu kuubembeleza upande wa pili.

Sudan inataka jina lake liondolewe katika orodha ya Marekani ya tawala zinazounga mkono ugaidi. Rais Donald Trump wa Marekani yeye yumo mbioni kuhakikisha kunakuweko uhusiano wa kawaida baina ya Waarabu na utawala haramu wa Israel kabla ya kufanyika uchaguzi wa Marekani mwezi ujao. Hivi sasa Rais wa Marekani ametangaza kuhusu kufikiwa makubaliano baina ya Khartoum na Washington na kwamba, jina la Sudan litaondolewa karibuni hivi katika orodha ya 'nchi zinazounga mkono ugaidi'. Trump amesema kuwa, mara  tu Marekani itakapopokea dola milioni 335 kama fidia ya Sudan kwa familia za wahanga wa mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani, jina la Sudan litaondolewa katika orodha ya 'tawala zinazounga mkono ugaidi'.

Sudan iliwekwa katika orodha ya Marekani ya mataifa yanayounga mkono ugaidi baada ya mashambulio dhidi ya kituo cha biashara cha kimataifa cha New York mwaka 1993. Licha ya kuwa Rais wa wakati huo wa Sudan Omar Hassan al-Bashir alifanya juhudi katika miaka yake ya mwisho ya uongozi kubadilisha siasa zake na kufuata sera za Marekani na waitifaki wake katika eneo, ili kwa njia hiyo jina la Sudan liondolewe katika orodha hiyo ya kigaidi, lakini hakufanikiwa katika hilo.

Abdalla Hamdouk, Waziri Mkuu wa Sudan

 

Baada ya matukio yaliyotokea katika anga ya siasa nchini Sudan na kuondolewa madarakani Omar al-Bashir, hivi sasa umepita takribani mwaka mmoja tangu serikali ya muda ichukue hatamu za uongozi chini ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdouk. Alipochukua wadhifa huo, Hamdouk alitangaza kuwa, miongoni mwa vipaumbele vyake ni kuondolewa jina la Sudan katika orodha ya Marekani ya 'nchi zinazounga mkono ugaidi'.

Hivi sasa Marekani na Sudan wameanzisha mchezo wa siasa wenye lengo la kusukuma mbele gurudumu la malengo yao. Viongozi wa Sudan wamo mbioni kunufaika na fursa kadiri inavyowezekana. Hilo linatokana na kuwa, vikwazo vya kifedha vya Marekani katika miaka ya hivi karibuni, kivitendo vimeifanya Sudan ikabiliwe na matatizo mengi ya kiuchumi.

Kupanda mno gharama za maisha, tatizo la ukosefu wa ajira na kuongezeka umasikini, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya kimaumbile kama mafuriko na hivi sasa kuenea virusi vya corona ni mambo ambayo yameifanya Sudan ikabiliwe na matatizo maradufu. Kudhamini chakula hususan ngano ndio daghadagha kuu ya viongozi wa nchi hiyo ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa watu milioni 9.6 nchini Sudan wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula.

Omar Hassan al-Bashir, Rais wa zamani wa Sudan

 

Katika upande mwingine, kwa sasa Sudan ina umuhimu wa aina yake kwa Trump. Mbali na kuwa na nafasi muhimu kijiografia na kuwa na utajiri, filihali Sudan inaweza kuwa karata ya turufu kwa Trump kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa Waarabu na utawala ghasibu wa Israel. Rais wa Marekani anafanya juhudi ili aitangaze Sudan kuwa nayo imetia saini makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel. Ili kufikia hilo, wakati ni muhimu sana kwa Trump hasa hivi sasa. Kimebakia kipindi cha chini ya wiki mbili kabla ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Marekani huku nafasi ya Trump ikiwa imedhoofika. Hivyo basi kujiunga Sudan na nchi za Bahrain na Imarati katika kuanzisha uhusiano na Israel inaweza kuwa karata ya turufu ya Trump kwa ajili ya kujijengea nafasi siku chache kabla ya uchaguzi.

Licha ya kuwa viongozi wa Sudan wanadai kuwa, walishalipa fidia hiyo iliyotakiwa na Mareekani na kwa hiyo jina la nchi hiyo litaondolewa katika orodha ya ugaidi, lakini kwa sasa kumekuwa kukiendelea majadiliano baina ya pande mbili huku kila upande ukitaka kupatiwa fursa na upendeleo fulani. Hata hivyo inaonekana kuwa, hatimaye Sudan itasalimu amri na kukubali takwa la Marekani  na hivyo kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel. Endapo viongozi wa Sudan watafuata mkumbo huo wa Bahrain na Imarat, inaonekana kuwa watakabiliwa na upinzani mkali wa ndani.

Pompeo alipokutana na Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok mjini Khartoum mapema mwezi uliopita wa Septemba

 

Abdul-Rahim Ali, Mkuu wa zamani wa Baraza la Fikihi ya Kiislamu sambamba na kuashiria upinzani wa akthari ya vyama vya siasa, taasisi na shakhsia watajika nchini Sudan dhidi ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ametangaza kuwa, kuanzisha hatua za kutekeleza uanzishaji uhusiano wa kawaiida na Israel kutakabiliwa na upinzani wa wananchi, kwani kufanya hivyo maana yake ni kuridhia kuendelea kuporwa zaidi ardhi za Wapalestina na kuzidi kupokonywa haki zao.

Katika upande mwingine, pamoja na kuwa kisheria Rais wa Marekani ana mamlaka ya kuyaondoa mataifa katika orodha ya kigaidi ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo, lakini uamuzi wake huo unapaswa kuungwa mkono na kupasishwa na Kongresi ya nchi hiyo.

Katika muda huu uliobakia hadi kufanyika uchaguzi nchini Marekani, inaonekana kuwa, Trump anafanya kila awezalo akitumia suhula zote ili kuhakikisha kuwa anawaridhirisha wapigakura ili wampe ridhaa ya kuongoza tena kupitia uchaguzi wa rais wa mwezi ujao nchini Marekani.

Tags

Maoni