Oct 22, 2020 07:54 UTC
  • Papa akosolewa kwa kubariki mahusiano na ndoa za watu wa jinsia moja

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amekosolewa vikali na makasisi wahafidhina wa kanisa hilo, kutokana na kauli yake inayoashiria kuwa anaunga mkono mahusiano na ndoa za watu wenye jinsia moja.

Mmoja wa viongozi wa Katoliki waliomjia juu Papa ni Askofu Thomas Tobin wa Providence, makao makuu ya jimbo la Rhode Island la Marekani ambaye amesema bayana kuwa: Taarifa ya Papa inapingana wazi wazi na mafundisho na msimamo wa muda mrefu wa Kanisa Katoliki juu ya mahusiano ya watu wenye jinsia moja. Askofu Tobin amesisitiza kuwa, kamwe kanisa hilo halitaruhusu au kubariki uozo wa namna hiyo wa kijamii.

Katika makala iliyorushwa hewani jana na Tamasha la Filamu la Rome, Papa ameonekana kuunga mkono ndoa za watu wa jinsia moja kwa kusema, "mabaradhuli wana haki ya kuwa katika familia, wao ni watoto wa Mungu. Huwezi kumfukuza mtu katika familia au kuyafanya maisha yake yawe mabaya kutokana na hili."

Katika makala hiyo, Papa amesema kinachopaswa kufanywa ni kuundwa sheria za kuwalinda watu walioko au wanaotaka kujiingiza katika mahusiano hayo ya watu wa jinsia moja.

Kanisa Katoliki linaandamwa na kashfa za ubaradhuli na baadhi ya maaskofu kuoa kisiri

Mapema mwaka huu, Kiongozi wa zamani wa Kanisa Katoliki Duniani Benedict XVI alimtaka Papa Francis kusitisha mpango wa Kanisa Katoliki wa kuruhusu wachungaji wenye wake kuwa makasisi na maaskofu wa kanisa hilo, mpango ambao Papa Francis anauunga mkono kutokana na kile kinachosemekana kuwa ni kupungua idadi ya viongozi wa kidini katika baadhi ya maeneo ya dunia kwa sababu ya kubanwa na sheria ya kutoruhusiwa kuoa.

Upinzani dhidi ya kuwepo makasisi wenye wake katika Kanisa Katoliki unaandamana na mashinikizo makubwa ya walimwengu kwa viongozi wa kanisa hilo kutokana na kashfa za ngono na udhalilishaji wa watoto wadogo unaofanywa na makasisi katika maeneo mbalimbali duniani.  

Maoni