Oct 23, 2020 02:51 UTC
  • Obama: Uongo na kutuhumu watu ndiyo mbinu kuu ya serikali ya Trump

Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani amemshutumu vikali rais wa hivi sasa wa nchi hiyo na kusisitiza kwamba, kusema uongo na kutuhumu watu wengine ndiyo sifa kuu ya Donald Trump na wasaidizi wake.

Obama amesema hayo katika hotuba yake mjini Philadelphia, Pennsylvania na huku akitangaza kwa mara nyingine kumuunga mkono Joe Biden, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi cha chama cha Democrats katika uchaguzi wa tarehe tatu mwezi ujao wa Novemba, amesema, tabia ya Trump ni kuwavunjia heshima na kuwatukana wapinzani wake na hata anatishia kuwafunga jela, tabia ambayo si ya kawaida kwa rais wa nchi.

Rais huyo wa zamani wa Marekani vile vile amegusia kukumbwa Trump na ugonjwa wa COVID-19 na kuongeza kuwa, Donald Trump hakuchukua hatua zinazotakiwa za kujikinga na maambukizo ya kirusi cha corona na hana uwezo wa kuchukulia mambo kwa uzito unaotakiwa.

Marais wa zamani na wa hivi sasa wa Marekani. Barack Obama (kulia) na Donald Trump

 

Uchaguzi wa rais nchini Marekani unazidi kukaribia. Zimebakia chini ya wiki mbili hadi kufanyika uchaguzi huo huku kura mbalimbali za maoni zikionesha kuwa mpinzani wa Trump, yaani Joe Biden wa chama cha Democrats anaongoza.

Siasa za kiuanagenzi na zenye utata mwingi, ufisadi wa kimaadili, hatua na maamuzi yasiyotabirika ya Trump na serikali yake, yote hayo yamechangia kupotea umaarufu wa rais huyo wa Marekani.

Udhaifu mkubwa aliouonesha Trump katika kukabiliana na mgogoro wa corona na kumbukumbu mbaya sana aliyojiwekea kama misimamo yake ya ajabu dhidi ya maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo, ni mambo ambayo yanaweza kiurahisi kumpokonya ushindi Trump katika uchaguzi wa mwanzoni mwa mwezi ujao.

Tags

Maoni