Oct 23, 2020 02:52 UTC
  • Mazoezi ya Kijeshi ya Japan, Marekani na Australia katika Bahari ya China Kusini

Kikosi cha Tano cha Jeshi la Majini la Marekani kimetangaza habari ya kuanza mazoezi ya kijeshi ya nchi hiyo na majeshi ya Japan na Australia katika maji ya Bahari ya China Kusini. Haya ni mazoezi ya tano ya kijeshi ya pamoja ya nchi hiyo katika Bahari ya China Kusini katika mwaka huu wa 2020.

Hapa linajitokeza swali kwamba, ni nini lengo la mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi ya Marekani na washirika wake wa Asia?

Wachambuzi wengi wa masuala ya siasa wanaona kuwa, Marekani na waitifaki wake wa Asia wanataka kutoa changamoto kwa Beijing kuhusu umiliki wa visiwa vya China vilivyoko katika bahari hiyo.

Uhusiano wa China na Marekani umeharibika sana katika kipindi cha sasa kuliko wakati wowote mwingine. Kwa sasa China na Marekani zimo katika vita kali inayoanzia kwenye vita vya kibiashara hadi kwenye masuala ya kiusalama. China inasisitiza kuwa, haitaki kuingizwa katika Vita Baridi vipya na Marekani, huku Washington ikizidisha mashinikizo yake dhidi ya Beijing. Katika mkondo huu imepangwa kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani wiki ijayo atafanya safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Kusini Mashariki mwa Asia kwa ajili ya kukabiliana na satua na ushawishi wa China katika eneo hilo. 

Mike Pompeo

Sambamba na kuongezeka harakati za Marekani Mashariki mwa Asia, waitifaki wa kijadi wa serikali ya Washington katika eneo hilo pia hawakukaa kimya. Waziri Mkuu wa Japan, Yoshihide Suga, katika safari yake ya kwanza nje ya nchi baada ya kushika hatamu za uongozi ameelekea katika nchi za Vietnam na Indonesia katika jitihada za kuimarisha uhusiano wa Tokyo na nchi za Kusini Mashariki mwa Asia. Safari hiyo inafanyika baada ya kikao cha nchi nne za India, Australia, Japan na Marekani kwa ajili ya kuanzisha muungano usio rasmi wa kukabiliana na ushawishi wa China katika eneo hilo. Sambamba na hayo, Japana inafanya mikakati ya kuzihamasisha nchi wanachama wa jumuiya ya ASEAN kwa ajili ya kuanzisha ushirikiano wa India na Pasific huru na ya wazi. 

Swala linaloonekana wazi ni kwamba, serikali ya Donald Trump imezidisha njama zake dhidi ya China katika kipindi hiki cha wiki mbili kabla ya uchaguzi wa rais nchini Marekani. Hata hivyo inatupasa kusisitiza hapa kwamba, tukiachilia mbali harakati za sasa za Trump za kutumia China kama turufu katika kampeni zake za uchaguzi wa rais, Washington imekuwa katika vita vya aina mbalimbali dhidi ya Beijing kwa muda sasa. Na kwa vile haikuweza kufikia malengo yake makuu katika uwanja huo, inafanya jitihada za kupanua vita hivyo katika nchi nyingi za Mashariki mwa Asia. Pamoja na hayo inatupasa kueleza kwamba, mienendo isiyo ya kidiplomasia ya Rais wa Marekani, na wasiwasi wa viongozi wa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia kuhusu tabia ya Donald Trump na serikali yake ya kutotekeleza ahadi na majukumu yake vinatatiza harakati za serikali ya Washington za kuanzisha muungano dhidi ya China katika eneo hilo. Hapa linakuja swali kwamba, ni kwa nini Marekani ina wasiwasi mkubwa na China?

Jibu la swali hili linapatikana katika uchambuzi wa jarida la The National Interest ambalo limeandika kuwa: Maendeleo makubwa ya China katika nyanja za uchumi na teknolojia vimeifanya nchi hiyo kuwa mpinzani wa Marekani na kuitia wahka Washington kuhusiana na nguvu hiyo kubwa ya kichumi duniani. 
Kwa ujumla inatupasa kusema kuwa, kwa sasa China ni miongoni mwa madola makubwa na inaelekea kushika nafasi ya Marekani duniani; suala ambalo linawatia kiherehere na wahka mkubwa wanastatejia na viongozi wa serikali ya Washington.       

Tags

Maoni