Oct 23, 2020 03:48 UTC
  • Zarif: Marekani inataka kuibua mashindano ya silaha duniani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Marekani kukataa kuongeza muda wa mkataba wa kupunguza silaha haribifu ni mfano wa wazi wa kutofungamana Marekani na mchakato wa kuleta uthabiti duniani na pia ni ishara ya nchi hiyo kuwa na hamu kubwa ya kuanzisha mashindano ya silaha duniani.

Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameyasema hayo Alhamisi usiku katika ujumbe aliouandika kwa lugha ya Kirusi katika ukurasa wake wa Twitter ambapo alisema:  "Hatua ya Marekani kukataa kurefusha muda wa Mapatano ya Kupunguza Silaha za Kistratijia SNV-III, ambayo ni kati ya mapatano muhimu zaidi kwa ajili ya usalama wa kimataifa na kudhibiti silaha, ambayo yanamalizika Februari 2020, ni mfano mwingine wa wazi kuhusu namna Marekani isivyotaka uthabiti duniani na pia ni mfano wa hamu kubwa ya nchi hiyo ya kuanzisha mashindano ya silaha duniani."

Ijumaa iliyopita, Rais Vladimir Putin wa Russia alipendekeza kurefushwa kwa mwaka mmoja muda wa mapatano ya kupunguza silaha baina ya Marekani na Russia bila masharti yoyote. Marekani impeinga pendekezo hilo.

Rais Putin amemuagiza waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov afuatilie kadhia hiyo ili kuweza kupokea jibu kamili la Marekani. Mapatano hayo ambayo  pia yanajulikana kama New START yalitiwa saini baina ya Marekani na Russia kwa lengo la kupunguza silaha haribifu za nyuklia.

Rais aliyepita wa Marekani Barack Obama na mwenzake wa Russia wakati huo Dmitry Medvedev walitia saini mapatano hayo mwaka 2010. 

Rais Vladimir Putin Russia amesema kuwa, endapo mkataba wa New START utavunjika na kutofikiwa makubaliano mapya, hakutakuwa tena na chombo cha kudhibiti ushindani wa silaha. Putin ametishia kuwa, kama Marekani haitaonyesha nia na ishara za kuongeza muda wa mkataba wa New START, basi Russia nayo itaruhusu mkataba huo ufikie tamati Februari mwakani.

Kufikia tamati kwa muda wa mkataba huo kutaifanya Marekani kwa mara nyingine tena ianze upanuaji wake wa silaha za nyuklia za kistratijia bila ya udhibiti wala mipaka yoyote ile, hatua ambayo itakabailiwa na jibu kutoka kwa Russia; na kwa utaratibu huo kutaongezeka ukosefu wa amani na uthabiti katika uga wa kimataifa na wakati huo huo kuibuka mashindano ya upanuaji silaha za nyuklia baina ya madola makubwa ya nyuklia ulimwenguni.

Tags

Maoni