Oct 23, 2020 07:26 UTC
  • Balozi wa Iran: Hatua za upande mmoja za Marekani zinahatarisha utawala wa sheria

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema uchukuaji maamuzi ya upande mmoja wa Marekani unahatarisha utawala wa sheria katika ngazi ya kimatiaifa.

Majid Takht-Ravanchi amesema hayo katika hotuba yake mbele ya Kamati ya Sita ya Kikao cha 75 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, mienendo hiyo ya Marekani inaiweka jamii ya kimataifa katika hali hatarishi.

Amesema tangu kuasisiwa Umoja wa Mataifa, suala la kuzishirikisha pande kadhaa katika kuchukua maamuzi limekuwa moja ya mafanikio makubwa katika mfumo wa UN.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, njia hiyo ya kufuata maamuzi ya pande kadhaa imechangia pakubwa katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani katika maeneo mbalimbali ya dunia. 

Makao makuu ya UN

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametaja baadhi ya hatua za upande mmoja za Marekani zinazohatarisha usalama, amani na uthabiti wa dunia kama uamuzi wa Washington wa kujiondoa katika mapatano ya kimataifa, kuanzisha vita vya kibiashara na nchi tofauti, ugaidi wa kiuchumi na kimatibabu kupitia vikwazo visivyo vya kibinadamu kwa malengo ya kisiasa na kuitishia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) pamoja na waendesha mashitaka wake.

Amesema mifano mingine ya hatua za upande mmoja za US zinazoyumbisha uthabiti wa dunia ni kuitumia kama silaha sarafu yake ya dola kuhujumu mfumo wa kimataifa wa fedha, kuziadhibu nchi zinazofuata maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuzuia mali na fedha za mataifa mengine, na vile vile kuwawekea vizuizi visivyo vya kiutu baadhi ya wawakilishi wa nchi wanachama wa UN.

 

Tags