Oct 23, 2020 13:12 UTC
  • Lawama na ukosoaji dhidi ya Marekani kwa kuyatuhumu mashirika matatu ya haki za binadamu kuwa eti yana chuki na Mayahudi

Katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake, Rais Donald Trump wa Marekani amechukua hatua nyingi kwa madhumuni ya kuitetea na kuiunga mkono Israel na kuyapiga vita mashirika ya kimataifa ambayo yamechukua msimamo wa kuwatetea na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina dhidi ya jinai wanazofanyiwa na utawala huo wa Kizayuni.

Katika mwendelezo wa hatua hizo, hivi sasa Washington inataka kuzitangaza asasi tatu za kutetea haki za binadamu, likiwemo tawi la Amerika la Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty Iternational, Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch na Shirika la Misaada la Oxfam kuwa ni mashirika "yenye chuki na Uyahudi". Kwa mujibu wa maafisa wawili rasmi wa Marekani, mnamo wiki hii Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo itatoa taarifa maalum itakayoelezea jinsi mashirika hayo yanavyowachukia Mayahudi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marejani Mike Pompeo ameunga mkono uamuzi huo; na jambo hilo limewafurahisha Wazayuni wakisema, linaendana na siasa na sera za Israel. Mashirika hayo matatu ya kutetea haki za binadamu yanatuhumiwa na Marekani kwamba yanaunga mkono Vuguvugu la BDS. Vuguvugu hilo la kimataifa la Boycott, Divestment and Sanctions linawaunga mkono Wapalestina kwa kuendesha kampeni dhidi ya Israel kwa kuisusia, kuitenga na kutoshirikiana nayo katika uwekezaji.

Maandamano ya Vuguvugu la BDS

Inavyoonyesha, Trump amechukua hatua hiyo akiwa na malengo mawili anayofuatilia. Kutokana na kukaribia tarehe ya kufanyika uchaguzi wa rais wa Marekani, na kwa kuzingatia kuwa Trump ameachwa nyuma na mshindani wake Joe Biden wa chama cha Democratic katika mbio za kinyang'anyiro hicho, hivi sasa anajaribu kwa kila njia kuongeza idadi ya wapigakura wake; na kwa ajili ya kufikia lengo hilo amechukua hatua hiyo ili mbali na kuvutia uungaji mkono wa lobi za Kizayuni za ndani ya Marekani, apiganie pia kupata kura nyingi zaidi za jamii ya Mayahudi, ambao kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, wengi wao wanamuunga mkono Biden.

Trump na Biden

Kama tulivyotangulia kueleza, katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake, Trump amechukua hatua nyingi kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni ikiwemo kujitoa Marekani katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na katika shirika la umoja huo la UNESCO kwa kisingizio kuwa, taasisi mbili hizo za UN zinachukua 'misimamo ya kiutashi dhidi ya Israel'. Kama alivyodai balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa  Nikki Haley ni kwamba: Lawama za kila mara za Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni kuhusiana na Wapalestina ni sababu nyengine iliyochangia kuchukuliwa uamuzi huo.

Kwa upande mwingine, hatua hiyo ya Trump inaonyesha kuwa Marekani haiwezi kuzivumilia hata taasisi za Kimagharibi za kutetea haki za binadamnu zinazoendesha shughuli zao kulingana na vigezo vya Magharibi; na kwa hiyo katika hatua ya kwanza inaziweka kwenye orodha ya makundi yanayopiga vita Mayahudi na kisha inachukua hatua ya kuziadhibu. Ukweli ni kwamba Washington huwa na mtazamo chanya kuhusiana na asasi za kimataifa za kutetea haki za binadamu pale tu utendaji wa asasi hizo unapokidhi maslahi ya Marekani na waitifaki wake ukiwemo utawala wa Kizayuni, lakini wakati asasi kama Amnesty International, Human Rights Watch na Oxfam zinapokosoa vitendo vya kinyama ambavyo Israel inawafanyia wananchi madhulumu wa Palestina kuanzia mauaji, kupora ardhi zao na kuwafukuza kwenye nchi yao ya asili ya tokea enzi za mababu zao, papo hapo Washington huzigeuzia kibao kwa kuzituhumu kuwa zina chuki na Mayahudi na kuchukua hatua dhidi yao.

Hata hivyo uamuzi huo wa Marekani umekosolewa vikali na mashirika hayo ya kutetea haki za binadamu ambayo mbali na kusikitishwa, yamekanusha pia tuhuma kwamba yana chuki na Mayahudi na yakasisitiza kuwa, kukosoa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel hakumaanishi kuwa na chuki na Mayahudi. Ni kama alivyoeleza afisa wa Human Rights Watch wa mjini New York Erick Goldstein kwamba "Kukosoa sera za serikali fulani, hakumaanishi kulishambulia kundi maalumu la watu." Kauli hiyo ya Goldstein inahusu ukosoaji wa shirika hilo la haki za binadamu kwa sera za Israel, jambo ambalo yeye anaamini haliwezi kuitwa hujuma dhidi ya Mayahudi.

Hatua inayochukuliwa na Washington dhidi ya mashirika matatu ya kimataifa ya haki za binadamu inaenda sambamba na hatua zilizochukuliwa na utawala wa Kizayuni pia, ambao katika miaka ya karibuni si tu umetoa vitisho vya kupiga marufuku shughuli za mashirika hayo lakini pia umewafukuza huko Tel Aviv baadhi ya maafisa wao.../

Tags

Maoni