Oct 24, 2020 04:19 UTC
  • Jaji wa Marekani ataka Bin Salman apandishwe kizimbani kwa jaribio na mauaji ya kigaidi

Jaji wa mahakama moja ya Marekani amemtaka mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman ajibu mashtaka ya tuhuma za kutaka kumuua kigaidi Saad al Jabri, mkuu wa zamani wa Idara ya Intelijensia la Saudi Arabia aliyekimbilia nchini Canada.

Jaji  Timothy J. Kelly wa Mahakama ya Federali ya Washington amemtaka Bin Salman kufika mahakamani na kujibu tuhuma za kutaka kumuua Saad al Jabri hadi kufikiia tarehe 7 Disemba. 

Tarehe Mosi Agosti mwaka huu Saad al Jabri ambaye pia alikuwa mshauri wa mrithi wa zamani wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Nayef, aliwasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya Muhammad bin Salman na maafisa wengine kadhaa wa serikali ya kifalme ya Saudi Arabia wakiwemo wasaidizi wakuu wa Bin Salman, Saud al Qahtani, Ahmed al Asiri na Badr al Asaker kwa tuhuma za kutaka kumuua kwa njia kama ile iliyotumiwa kumuua mwandishi na mkosoaji wa utawala wa Riyadh, Jamal Khashoggi. 

CIA: Bin Salman aliamuru mauaji ya Jamal Khashoggi

Mashtaka hayo pia yamesisitiza kuwa Idara ya Upelelezi ya Marekani imezima jaribio la kutaka kumuua al Jabri nchini Canada baada ya kuwasiliana na serikali ya nchi hiyo.

Saad al-Jabri, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Canada na anayejulikana kama "Kisanduku Cheusi cha Aal Saud", ana nyaraka muhimu zinazomhusu mfalme Salman bin Abdul-Aziz pamoja na mwanawe Muhammad bin Salman ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo ambapo kama nyaraka hizo zitavuja na kusambazwa zinaweza kuharibu mno haiba ya bin Salman ulimwenguni.  

Tags

Maoni