Oct 24, 2020 11:08 UTC
  • Wasiwasi wa Amnesty International kuhusu ghasia na machafuko katika kampeni za uchaguzi Marekani

Kupamba moto kampeni za uchaguzi nchini Marekani kwa katika kipindi hiki cha kukaribia tarehe ya uchaguzi wa rais hapo Novemba 3 mwaka huu, na jitihada za Rais Donald Trump wa nchi hiyo ambaye ni mgombea wa chama cha Republican za kutaka kuzusha hali ya mvutano katika jamii ya Marekani, vimeibua hali ya wasiwasi.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza wasiwasi wake mkubwa kutokana na matukio ya ghasia na machafuko katika mikutano ya kampeni za uchaguzi nchini Marekani. Shirika hilo limetangaza katika ripoti yake kwamba askari usalama wa Marekani hivi sasa hawana uwezo wa kuzuia harakati za kuvuruga mikusanyiko ya amani na kwamba, usalama wa wafanya maandamano na wapiga kura katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Donald Trump huko Marekani hauna dhamana. Shirika hilo limekitaja chanzo kikuu cha machafuko na vitendo vya ghasia katika kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani kuwa ni watu wenye silaha; na limeinasihi serikali ya Marekani kuzuia ubebaji silaha katika maeneo ya umma, mabustanini na katika vituo vya kupigia kura na vilevile katika mikusanyiko ya amani inayohusiana na uchaguzi.  

Ghasia katika kampeni za uchaguzi wa rais Marekani 

Jitihada za Trump za kuzusha mivutano katika kipindi hiki cha uchaguzi huko Marekani kwa madai ya kufanyika udanganyifu katika zoezi la upigaji kura kwa njia ya posta na pia kuwatuhumu magavana na wakuu wa majimbo wa chama cha Democratic kuwa wametupilia mbali kura zake mara kadhaa, na vilevile kutishia kuwa hataondoka madarakani iwapo atashindwa katika uchaguzi huo, kuwachochea wafuasi wake kumiminika mitaani wakiwa na silaha na kisha kuishambulia mikutano na kampeni za wapinzani wake, ni kati ya sababu kuu machafuko, ghasia na ukosefu wa usalama ambao haujawahi kushuhudiwa huko Marekani. Adam Schiff Mkuu wa Kamati ya Intelijinsia Katika Bunge la Wawakilishi la Marekani amesema:  Hatua na mienendo ya Rais Trump ndio sababu ya kushtadi vitendo vya ghasia nchini.  

Adam Schiff, Mkuu wa Kamati ya Intelijinsia Katika Bunge la wawakilishi la Marekani 

Kati ya mwezi Mei hadi Septemba mwaka huu 2020 asilimia 75 ya mikutano ya kampeni za uchaguzi imegubikwa na vitendo vya ghasia na mapigano kote nchini Marekani. Jambo lililo na umuhimu ni kuwa polisi ya Marekani, kwa makusudi au la, haichukui hatua madhubuti za kuzuia hali hii ya machafuko ambayo imekuwa changamoto kuu. Kwa mfano, katika visa zaidi ya 12 vilivyochunguzwa, polisi ya Marekani haikuwepo kwa muda mrefu au haikuonekana kabisa katika maeneo ya matukio hayo.  

Wakati huo huo hivi sasa jamii ya Marekani imekuwa jamii yenye kambi mbili kwa kuzingatia malumbano na mpambano mkali unaoshuhudiwa baina ya wagombea wawili wa kiti cha urais nchini humo yaani Donald Trump, anayepeperusha bendera ya chama cha Republican, na Joe Biden wa chama cha Democratic; huku jamii hiyo ikismbuliwa na wimbi la ghasia na machafuko. Kuanzia sasa polisi imepiga marufuku uwepo wa watu wenye silaha karibu na maeneo ya uchaguzi katika baadhi ya majimbo wakati wa kufanyika uchaguzi huo wa rais, ikihofia uwezekano wa kujiri mapigano kati ya wafuasi wa wagombea hao wawili.  

Joe Biden, mpinzani mkuu wa Trump katika uchaguzi ujao wa Rais 

Inatabiriwa kuwa iwapo matokeo ya uchaguzi wa rais hayatakuwa kwa maslaji ya Trump na kiongozi huyo akapinga namna uchaguzi huo uliovyoendeshwa sambamba na kudai kufanyika udanganyifu, na suala hilo likawasilishwa kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua kama ya kuhesabiwa upya kura katika majimbo yenye upinzani mkali au faili hilo likafikishwa katika Mahakama za Federali au Mahakama Kuu ya Marekani; wafuasi wa Trump ambao wanachochea machafuko, watasababisha ghasia kubwa na hali ya mchafukoge ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miji na majimbo ya nchi hiyo. Iwapo yatajiri hayo, Marekani inaweza kutumbukia katika zama za ghasia kubwa, hali ya mchafukoge na hata vita vya ndani.

Kuhusiana na suala hilo, Baraza la Uhusiano wa Nje la Marekani limetangaza kuwa baadhi ya waungaji mkono wa Trump na wanamgambo waliojizatiti vyema vya silaha wamedhamiria kufanya fujo iwapo Trump atashindwa katika uchaguzi ujao. 

Tags

Maoni