Oct 25, 2020 08:03 UTC
  • UN yatangaza kuanza kutekelezwa mkataba wa kuzuia silaha za nyuklia

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa nchi nyingine 50 zimepasisha utekelezaji wa mkataba unaopiga marufuku silaha za nyuklia.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa nchi 50 duniani zimepasisha utekelezaji wa mkataba unaopiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia (TPNW) huku uwanja wa kutekeleza makubaliano hayo ukiandaliwa hadi kufikia siku 90 nyingine.  Inatazamiwa kuwa mkataba huo utaanza kutekelezwa Januari mwakani. 

Thailand, Mexico, Afrika Kusini, Bangladesh, New Zealand, Vietnam, Honduras na Vatican ni kati ya nchi ambazo hadi sasa zimepasisha mkataba huo.  

Taasisi nyingine zisizo za kiserikali ikiwemo Harakati ya Kimataifa ya Kuangamiza Silaha za Nyuklia ambayo mwaka 2017 ilishinda tuzo ya Amani ya Nobel, zimekaribisha suala la kuandaliwa uwanja wa kutekelezwa mkataba huo. Wakati huo huo, Marekani wiki iliyopita iliziandikia nchi zilizosaini mkataba huo unaopiga marufuku silaha za nyuklia ikizitaka kujitoa katika mkataba huo. 

Silaha za nyuklia za Marekani 

Mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia ulipasishwa tarehe 7 Julai mwaka 2017 na nchi 122 katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Iran ni miongoni mwa nchi zilizoupigia kura ya ndio mkataba huo.

Nchi zinazomiliki silaha za nyuklia na waitifaki wao ikiwemo Uholanzi zimeupigia kura ya hapana mkataba huo. Mkataba huo unazitaka nchi zilizousaini kutoimarisha silaha za nyuklia au zana nyingine za milipuko, kutozifanyia majaribio au kuziunda, kutozihifadhi au kuzimiliki katika mazingira yoyote yale. 

Tags

Maoni