Oct 25, 2020 12:51 UTC
  • Recep Tayyip Erdoğan
    Recep Tayyip Erdoğan

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa Rais wa Ufaransa, Emanue Macron, anahitaji kupimwa uwezo wake wa kiakili baada ya matamshi ya kibaguzi aliyotoa karibuni kuhusu dini ya Uislamu.

Recep Tayyip Erdoğan aliyekuwa akihutubia mkutano wa chama tawala cha Uadilifu na Ustawi nchini Uturuki amehoji kwamba: "Ni kitu gani tunaweza kusema kuhusiana na rais wa nchi asiyejua maana ya uhuru wa itikadi na anaamiliana na mamilioni ya wafuasi wa dini tofauti (Uislamu) nchini kwake kwa njia kama hii?"

Rais wa Uturuki amesema: "Hivi kweli Rais Macron wa Ufaransa ana tatizo gani na Uislamu na Waislamu? Anahitaji kupewa matibabu ya matatizo ya akili".  

Recep Tayyip Erdoğan amesema kuwa, Ufaransa itafanya uchaguzi wa rais yapata mwaka mmoja ujao ambao utaainisha hatima ya Macron, na kwamba anaamini utakuwa mwisho wake kwa sababu hajaifanya lolote Ufaransa seuze nafsi yake mwenyewe.

Mapema mwezi huu na katika mwendelezo wa sera za kupiga vita Uislamu nchini Ufaransa, Emmanuel Macron alizindua mpango wa eti kulinda thamani za kisekulari za nchi hiyo dhidi ya kile kilichotajwa kama "Misimamo Mikali ya Kiislamu".

Emmanuel Macron 

Rais wa Ufaransa alidai kuwa Uislamu ni dini iliyo "kwenye mgogoro" ulimwengu mzima, matamshi ambayo yamewaghadhabisha Waislamu kote duniani.

Emmanuel Macron pia ameunga mkono kitendo kiovu cha jarida la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (SAW) na kusisitiza kuwa, Ufaransa itaendelea kuchapisha vibonzo hivyo. Macron amedai kuwa huo ni uhuru wa kujieleza.

Tags

Maoni