Oct 26, 2020 02:31 UTC
  • Uchaguzi wa 2020 Marekani; uchaguzi usiotabirika

Harakati za taasisi za uchunguzi wa maoni zimeongezeka sana katika wakati huu wa kukaribia kuingia wiki ya mwisho ya kampeni za uchaguzi wa rais nchini Marekani, wa Novemba 3, 2020.

Katika kipindi cha siku za hivi karibuni, taasisi nyingi za uchunguzi wa maoni zimekuwa zikionesha kuzidi kupungua asilimia ya nafasi ya ushindi baina ya Donald Trump wa chama cha Republican na Joe Biden wa chama cha Democratic hasa katika majimbo muhimu zaidi ambayo yamepachikwa jina la uwanja wa mapambano. Pamoja na hayo, bado Joe Biden anaongoza katika uchunguzi huo wa maoni. Ukiangalia wastani wa uchunguzi mbalimbali wa maoni utaona kuwa Biden yuko mbele kwa asilimia nane ikilinganishwa na Trump.

Pamoja na hayo, uchunguzi huo wa maoni si dhamana ya ushindi kwa mgombea wa chama cha Democratic kwani hata katika uchaguzi wa mwaka 2016, mgombea wa chama hicho alishinda kwa kura nyingi za wananchi, lakini Trump alitumia hila ya kura za "Electoral College" akatangazwa mshindi wa uchaguzi huo.

Uchunguzi wa maoni jimbo la Pennsylvania huko Marekani

 

Tab'an mizozo na mivutano ya kisiasa iliyoigubika Marekani hivi sasa imezidisha utata katika utabiri wa matokeo ya uchaguzi huo. Mara chungu nzima Trump amekuwa akiashiria kuwa hatokubali matokeo ya kura ambayo hayatomtangaza yeye mshindi. Kwa maneno mengine ni kuwa, kama Trump atashindwa, basi timu yake itatoa madai ya kuweko udanganyifu katika uchaguzi huo na kufungua kesi mahakamani, mahakama ambayo tayari Trump ameshaweka watu wake wa kumtangaza mshindi. Inaonekana wazi kwamba mara hii Trump ameelekeza matumaini yake kwa Mahakama Kuu ya Marekani ambayo inadhibitiwa na watu wake.

Hata iwapo kura za "Electoral College" hazitofanikiwa kumpata mshindi yaani kama mgombea atakosa kwa uchache kura 270, na jukumu la uchaguzi wa baadaye kuingia mikononi mwa Baraza la Congress bado Trump atakuwa na nafasi ya kushinda licha ya kwamba wanachama wa chama cha Democratic ni wengi kwenye baraza hilo. Sababu yake ni kwamba, wakati wa upigaji kura kila jimbo litakuwa na kura moja tu ambapo katika upande huo, idadi ya majimbo yenye wabunge wengi wa Republican ni mengi ikilinganishwa na ya chama cha Democratic.

Wanamgambo wabaguzi wakubwa wa rangi walioambiwa na Trump wajiweke tayari kwa lolote

 

Kiujumla ni kwamba ni vigumu kutabiri mshindi katika uchaguzi ujao wa rais wa Marekani kwani mfumo wa uchaguzi nchini humo una mazonge mengi. Hata hivyo jambo moja liko wazi nalo ni kwamba uchaguzi wa tarehe 3 Novemba 2020 nchini Marekani hautopita salama. Tayari hatua kali za kiusalama zimeshachukuliwa mapema katika baadhi ya miji ya Marekani ili kukabiliana na machafuko ya baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi. Katika baadhi ya maeneo tayari kumepigwa marufuku kubeba silaha katika maeneo ya upigaji kura. Matamshi ya kichochezi ya Trump kama yale aliyoyatoa katika mdahalo wa kwanza kati yake na Joe Biden akiwataka wanamgambo wake wenye misimamo mikali ya kuhisi wazungu ni bora kuliko watu wengine wajiweke tayari kwa lolote, ni ishara nyingine inayothibitisha kwamba uchaguzi wa tarehe 3 Novemba 2020 huko Marekani hautopita salama.

Terence Monahan, kamanda wa jeshi la polisi wa New York amesema: Ni jambo lisilo na shaka kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na vurugu zaidi ikilinganishwa na chaguzi za huko nyuma na ndio maana tumejiandaa kukabiliana na hali yoyote ile.

Sababu nyingine inayotilia nguvu uwezekano wa kutokea mapigano na machafuko nchini Marekani baada ya uchaguzi wa tarehe 3 Novemba 2020 ni uzoefu wa chaguzi zilizopita ambazo zilijaa tuhuma za kuvurugwa na mikono ya ndani na nje ya Marekani. Baada ya uchaguzi wa tarehe 3 Novemba, chama kilichoshindwa kitaweza kiurahisi kulalamikia kuporwa ushindi na kutokubali matokeo suala ambalo litazidi kuisambaratisha jamii ya Marekani.