Oct 26, 2020 02:33 UTC
  • Ununuzi wa silaha waongezeka Marekani kwa kiwango cha kutisha wakati wa kukaribia uchaguzi wa rais

Kuongezeka ununuzi wa silaha kwa kiwango cha kutisha nchini Marekani kumezidisha hofu na wasiwasi wa kuzuka machafuko baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

Hisia za kukabiliwa na hatari zimezidi kuongezeka miongoni mwa Wamarekani kutokana na yale yanayoweza kujiri nchini humo katika siku zijazo kwa sababu ya hofu na wasiwa kwamba baadhi ya watu wanaweza kutumia silaha moto kulalamikia matokeo ya zoezi la upigaji kura katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo utakaofanyika Novemba 3.

Hii ni baada ya kukamatwa pia kijana wa miaka 19 anayedaiwa kula njama ya kumuua Joe Biden, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Polisi ya Marekani ilimkamata kijana huyo katika eneo la kilomita chache kutoka kwenye nyumba ya Biden katika jimbo la Carolina Kaskazini, ambapo iligundua pia ndani ya gari lake silaha za aina mbali mbali na orodha ya watu ambao kwa mujibu wa yeye inapasa wauawe.

Joe Biden

Ripoti za vyombo vya habari kuhusiana na hali hiyo zinatolewa wakati makundi wa wazungu wabaguzi wa rangi wanajiona bora yamejizatiti vikali kwa aina mbali mbali za silaha moto.

Mengi ya makundi hayo yanamuunga mkono Rais wa Marekani Donald Trump na yameshaonya kuwa yatachukua hatua endapo Trump atashindwa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais.

Matokeo ya chunguzi nyingi za maoni zilizofanywa hivi karibuni yanaonyesha kuwa mshindani mkuu wa Trump, Joe Biden ana nafasi kubwa zaidi ya kushinda uchaguzi huo.../

Tags

Maoni