Oct 26, 2020 03:22 UTC
  • Waislamu wahimizwa kususia bidhaa za Ufaransa
    Waislamu wahimizwa kususia bidhaa za Ufaransa

Malalamiko na ukosoaji dhidi ya matamshi yaliyotolewa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akitetea vitendo vya kutusiwa na kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad (saw) nchini humo unaendelea kupamba moto huku nchi mbalimbali za Kiislamu zikitoa wito wa kuiadhibu Paris kwa kususia bidhaa za Ufaransa.

Katika uwanja huo Rais Emmanuel Macron alijitokeza tena jana bila ya soni na kutetea tena matusi na kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu kwa kuandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba, Paris haitalegeza kamba wala kurudi nyuma. 

Rais wa Ufaransa amedai kuwa, hakubali matamshi yanayochochea chuki na kwamba anatetea mijadala ya kimantiki.

Wakati huo huo Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa imetoa taarifa ikizitaka nchi za Waislamu kusitisha wito wa kususiwa bidhaa za nchi hiyo baada ya Rais Macron kutetea matusi na vitendo vya kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad (saw) katika jarida la Charlie Hebdo la nchi hiyo. 

Kwa sasa trend inayotamba katika mitandao ya kijamii kwenye nchi za Kiislamu ni ile ya "#Susia Bidhaa za Ufaransa" kama jibu la awali dhidi ya matamshi ya rais wa nchi hiyo ya kutetea matusi na kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad (saw). 

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan amejibu jeuri ya Rais wa Ufaransa akisema: Macron amehujumu Uislamu baada ya kuhamasisha vibonzo vinavyomtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw).

"Inasikitisha kuona Rais wa Ufaransa akiamua kuzijeruhi nyoyo za mamilioni ya Waislamu wakiwemo raia wa nchi yake mwenyewe kwa kuhamasisha vibonzo vinavyouvunjia heshima Uislamu na Mtume wetu (saw)", amesema Imran Khan.

Spika wa Bunge la Kuwait Marzouq Al-Ghanim pia amelaani vikali hatua ya jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa ya kuchapisha tena vibonzo vinavyodhalilisha Mtume Muhammad (saw) na ameitaka serikali ya nchi hiyo kupiga vita kitendo chochote cha makusudi kinachovunjia heshima misingi ya Uislamu.

Kwa upande wake Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa Rais wa Ufaransa, Emanue Macron, anahitaji kupimwa uwezo wake wa kiakili baada ya matamshi ya kibaguzi aliyotoa karibuni kuhusu dini ya Uislamu.

Recep Tayyip Erdoğan amehoji: "Ni kitu gani tunaweza kusema kuhusiana na rais wa nchi asiyejua maana ya uhuru wa itikadi na anaamiliana na mamilioni ya wafuasi wa dini tofauti (Uislamu) nchini kwake kwa njia kama hii?"

Rais wa Uturuki amesema: "Hivi kweli Rais Macron wa Ufaransa ana tatizo gani na Uislamu na Waislamu? Anahitaji kupewa matibabu ya matatizo ya akili". 

Muhammad Ali al Houthi amelaani vikali kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad (saw) nchini Ufaransa na amezitaka nchi za Kiislamu kuitisha kikao rasmi cha kulaani uhalifu huo.

Mashirika na maduka makubwa katika baadhi ya nchi za Kiislamu kama Kuwait na Qatar tayari yameanza kutekeleza wito wa kususiwa bidhaa za Ufaransa kama hatua ya mwanzo na kuitia adabu Paris baada ya rais wa nchi hiyo kutetea uovu wa kuvunjiwa heshima al Habib, Muhammad (saw).

Tags

Maoni