Oct 26, 2020 08:34 UTC
  • Mvutano mpya baina ya Ufaransa na Uturuki baada ya Paris kuendeleza hujuma dhidi ya Uislamu

Uhusiano wa nchi mbili za Ufaransa na Uturuki umekumbwa na miivutano mingi katika miezi ya karibu kutokana na kuhitilafiana katika masuala kadhaa zikiwemo harakati za Uturuki huko Mashariki mwa Bahari ya Mediterania.

Hata hivyo jambo lililotibua zaidi uhusiano wa Ankara na Paris ni hatua ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ya kuendeleza hujuma na mashambulizi dhidi ya Uislamu na Waislamu. Mgogoro na mivutano kati ya pande hizo mbili imepamba moto baada ya matamshi yaliyotolewa juzi na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki akijibu hujuma ya Macron. Baada ya matamshi hayo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa imemwita balozi wa Uturuki nchini humo na kumkabidhi malalamiko ya Paris dhidi ya Ankara. Jumamosi iliyopita Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alilaani hujuma ya jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo ya kuchapisha tena vibonzo vinavyodhalilisha na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) na matamshi ya Macron ya kutetea na kuhamasisha kitendo hicho. Erdogan alihoji kwamba: "Hivi kweli Rais Macron wa Ufaransa ana tatizo gani na Uislamu na Waislamu? Anahitaji kupewa matibabu ya matatizo ya akili".  

Erdogan alisema: "Hatua ya Ufaransa, ambayo bado inajinadi kuwa ngome ya uhuru na misimamo ya kisekulari, ya kuchora tena vibonzo vinavyomtusi Mtume Muhammad (saw) ni uovu mbaya zaidi na haioani na misingi ya uhuru; kinyume chake, inahesabiwa kuwa ni hujuma dhidi ya Uislamu." 

Macron

Hatua ya mwalimu mmoja wa Ufaransa ya kuwaonyesha wanafunzi wake vibonzo vinavyomtusi Mtume Muhammad (saw) darasani, na kuuliwa mwalimu huyo na kijana mmoja mwenye asili ya Chechnia vimeakisiwa kwa kiwango kikubwa katika magazeti na vyombo vya habari vya nchi hiyo. Baada ya matukio hayo serikali ya Ufaransa imezidisha ukandamizaji dhidi ya jamii ya Waislamu na kuanza kufunga baadhi ya misikiti sambamba na kuchukua uamuzi wa kuwafukuza mamia ya Waislamu nchini humo. Hali imekuwa mbaya kwa Waislamu wa Ufaransa kiasi kwamba, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ameeleza kusikitishwa kwake na uwepo wa sehemu ya kuuza vyakula halali katika maduka ya nchi hiyo!

Vilevile Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kwa jeuri kwamba nchi hiyo itaendelea kusambaza katuni na vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (saw).

La kushangaza ni kuwa Ufaransa imemwita na kumsaili balozi wa Uturuki mjini Paris baada tu ya matamshi yaliyotambuliwa na serikali ya Paris kuwa yana harufu ya kudhalilisha yaliyotolewa na Rais Erdogan wa Uturuki. Mchambulizi wa masuala ya kisiasa Dokta Abdullah Ganji anasema: "Siku chache zilizopita huko Ufaransa walimvunjia heshima na kumdhalilisha Mtume Muhammad (saw) na wakati huo Rais Emmanuel Macron alikitaja kitendo hicho kuwa ni uhuru wa kujieleza na kusema. Sasa Recep Tayyip Erdoğan ametoa tamko lililotambuliwa kuwa ni kumvunjia heshima Macron, na muda kidogo baadaye balozi wa Uturuki aliitwa na kusailiwa. Hii ina maana kwamba, katika uhuru wa kusema na kujieleza wa nchi za Magharibi marais wa nchi wana heshima na hadhi kubwa zaidi kuliko Mtume wa Mwenyezi Mungu anayefuatwa na watu zaidi ya bilioni moja na nusu."

Mwenendo wa kuhujumu Uislamu na kuchezea shere matukufu ya dini hiyo na wafuasi wake wanaounda asilimia karibu 10 ya Wafaransa wote, umeshadidi sana katika miaka ya karibuni. Vilevile serikali ya Paris imezidisha mashinikizo dhidi ya jamii ya Wislamu kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo mikali.

Kwa sasa Ufaransa imekuwa kituo kikuu cha propaganda chafu za kutia doa sura safi ya Uislamu na kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw), na jambo hilo limepingwa vikali ya Waislamu. Wafaransa wanaweka mbele suala la uhuru wa kusema na kujieleza wakati wanapozungumzia Uislamu na matukufu yake, ilhali Ufaransa hiyo hiyo inawafunga na kuwasweka jela watu na hata wasomi wanaoeleza mitazamo yao ya kisayansi au hata kuhoji idadi ya Wayahudi wanaodaiwa kuuliwa katika Vita vya Pili vya Dunia (Holocaust)!

Hujuma dhidi ya Uislamu hususan kuchapishwa tena vibonzo vinavyomtusi na kumdhalilisha Mtume Muhammad (saw) imewakasirisha sana Waislamu wenye mwamko kote duniani. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa taarifa kali ikieleza kustaajabishwa na matamshi ya baadhi ya viongozi rasmi wa Ufaransa na kusisitiza kuwa, kuendelea kutolewa matamshi kama hayo kutakutavuruga uhusiano wa Ufaransa na nchi za Kiislamu na kuzidisha chuki na uhasama.

Wakati huo huo mashirika na maduka makubwa katika baadhi ya nchi za Kiislamu kama Kuwait na Qatar tayari yameanza kutekeleza wito wa kususiwa bidhaa za Ufaransa kama hatua ya mwanzo na kuitia adabu Paris baada ya rais wa nchi hiyo kutetea uovu wa kuvunjiwa heshima al Habib, Muhammad (saw).

Kwa sasa trend inayotamba katika mitandao ya kijamii kwenye nchi za Kiislamu ni ile ya "#Susia Bidhaa za Ufaransa" kama jibu la awali dhidi ya matamshi ya rais wa nchi hiyo ya kutetea matusi na kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad (saw).

Tags

Maoni