Oct 27, 2020 02:27 UTC
  • Msimamo wenye utata wa Gulbuddin Hekmatyar kuhusu kuundwa serikali ya muda Afghanistan

Mkuu wa chama cha Kiislamu cha Afghanistan katika msimamo wake uliozusha utata na mjadala amesema kuwa njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ni kuunda serikali ya muda.

Gulbuddin Hekmatyar amesema katika mkutano na vyombo vya habari kwamba, kundi la Taliban haliikubali serikali ya sasa ya Afghanistan inayoongozwa na Muhammad Ashraf Ghani; na  kwamba njie pekee ya kutatua matatizo ya nchi hiyo ni kuunda serikali ya muda. Mkuu wa chama cha Kiislamu cha Afghanistan ameongeza kuwa, Pakistan imemuhakikishia kuwa itafanya kazi kwa uaminifu katika mchakato wa mazungumzo ya amani ya Afghanistan. Gulbuddin Hekmatyar siku kadhaa zilizopita alifanya ziara nchini Pakistan na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo akiwemo Waziri Mkuu Imran Khan. Maoni na mitazamo ya kutilia maanani ya Gulbuddin Hekmatyar kuhusu kuunda serikali ya muda ili kuindoa Afghanistan katika hali ya mgogoro ni kadhia ambayo mpango wake karibu miaka miwili iliyopita ulikabiliwa  na radiamali kali nchini humo. 

Mkuu wa chama cha Kiislamu cha Afghanistan amedhihirisha msimamo wake huo katika hali ambayo safari yake huko Pakistan na mazungumzo aliyofanya na baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hyo yametajwa na badhi ya duru za Afghanistan kuwa ni juhudi zenye lengo la kuiondoa madarakani serikali ya sasa ya nchi hiyo. Hasa ikizingatiwa kuwa katika ziara yake mjini Islamabad Hekmatyar aliituhumu serikali ya Afghanistan kuwa inavuruga mwenendo wa amani na kueleza kuwa serikali ya Ashraf Ghani inataka kuendeleza vita na kuwa haiungi mkono amani. 

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan 

"Nusrat Rahimi" Msemaji wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan ametoa radiamali yake kwa safari rasmi ya Gulbuddin Hekmatyar Mkuu wa Chama cha Kiislamu cha Afghanistan nchini Pakistan ambapo ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Hekmatyar ana malengo sumu katika safari hiyo; kwa msingi huo njama zake zinapaswa kuzimwa. Hekmatyar angali anawaza kupata madaraka kupitia njia haramu na zisizo za kisheria.   

Safari ya Hekmatyar nchini Pakistan imefanyika katika hali ambayo hana wadhifa wowote rasmi katika serikali ya Afghanistan; na alikuwa mpinzani wa Muhammad Ashraf Ghani katika uchaguzi uliopita wa rais wa nchi hiyo. Matamshi yaliyozusha kelele ya Hekmatyar katika safari yake huko Pakistan ambapo ameituhumu serikali ya Afghanistan kuwa inakwamisha mchakato wa amani yanatathminiwa kuwa kinyume na malengo yaliyotangazwa ya safari yake hiyo kuhusu kufanya mashauriano na viongozi wa Islamabad ili kusaidia kurejesha amani huko Afghanistan. 

Msimamo wa Hekmatyar mbele ya vyombo vya habari kuhusu kuundwa serikali ya muda  unaweza kumfanya mkuu huyo wa chama cha Kiislamu kuzidi kukosolewa, mbali na safari yake huko Pakistan na msimamo wake mkali dhidi ya serikali ya Ashraf Ghani kukabiliwa na radiamali kali ndani ya Afghanistan. 

Kabla ya hili pia, suala la kuunda serikali ya muda huko Afghanistan lilizungumziwa na Zalmay Khalil Zad Mjumbe Maalumu wa Marekani katika Masuala ya Afghanistan katika mchakato wa mazungumzo kati ya Washington na Taliban na kupingwa vikali na wananchi, serikali na baadhi ya vyama vya Kiafghani. 

Hamdullah Moheb Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa Afghanistan ndiye aliyekosoa vikali mpango wa Khalil Zad kuhusu kuundwa serikali ya muda nchini humo. Hamdullah Muheb alikosoa vikali mpango wa kuasisi serikali ya muda nchini Afghanistan uliopendekezwa na Khalil Zad na kuutaja kuwa ni katika fremu ya siasa za White House za kudhoofisha serikali ya nchi hiyo. Kutolewa radiamali hasi kama hizo kwa mpango wa kuunda serikali hiyo ya muda kuliipelekea Marekani kuachana na mpango huo wa kutiliwa shaka. 

Hamdullah Moheb, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Afghanistan 

Kwa kuzingatia tajiriba ya upinzani mkubwa kwa mpango wa kuunda serikali ya muda huko Afghanistan swali hili linaulizwa kwamba je, ni kwa nini Hekmatyar kwa mara nyingine tena amezungumzia kuhusu mpango huo wenye utata? Hapa kuna dhana hii kuwa, Hekmatyar ana matumaini kwamba kwa kuundwa serikali hiyo ya muda ataweza kushirikishwa katika nyadhifa muhimu za madaraka katika mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo.  

Huenda ni kwa kutegemea senario kama hiyo ndipo siku kadhaa zilizopita Hekmatyar aliwalisha pendekezo la kuungana na Taliban huko Afghanistan; hata hivyo kundi hilo halijatoa jibu lolote katika uwanja huo. 

Hekmatyar ametoa pendekezo hilo la kuundwa serikali ya muda ili kuiondoa Afghanistan katika hali ya mgogoro huku takwa kuu la kundi la Taliban katika mazungumzo ya Qatar likiwa ni kutekelezwa ahadi ya Marekani ya kuondoka kikamilifu huko Afghanistan. 

      

Tags