Oct 27, 2020 06:04 UTC
  • Kukiri Marekani kuishiwa na vikwazo vya kuipigisha magoti Iran

Baada ya rais wa Marekani kutangaza kuitoa nchi yake katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei 2018 na kuirejeshea Iran vikwazo vyote ilivyokuwa imeondolewa baada ya mapatano hayo, Donald Trump na serikali yake walidhani kwa njia hiyo wataweza kutimiza kiurahisi ndoto yao ya kupigisha magoti Tehran na kuilazimisha ikubali mapatano yanayotakiwa na Washington. Hata hivyo ndoto hiyo kamwe haikuaguka.

Sasa hivi viongozi wa Marekani wanakiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba vikwazo vyao vimeshindwa. Matamshi ya karibuni kabisa ya kukiri huko ni yale yaliyotolewa na Robert O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani ambaye amesema, kapu la vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran limeshabakia tupu na imeishiwa na vikwazo vya kuifanya Jamhuri ya Kiislamu isalimu amri.

Akijibu swali kuhusu madai ya kuingilia Iran na Russia uchaguzi wa Marekani na hatua ambazo Washington inapanga kuzichukulia nchi hizo mbili, O'Brien amesema: "Miongoni mwa matatizo tuliyo nayo sasa hivi ni kwamba hadi hivi sasa Marekani imeshaziwekea Iran na Russia vikwazo vikubwa sana na unapoangalia kiundani utaona hakuna vikwazo zaidi ambavyo vinaweza kutumiwa kama silaha yenye taathira dhidi ya nchi hizo mbili." Pamoja na hayo amesema, White House inafikiria njia zozote zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya nchi tatu za Iran, Russia na China.

Rais wa Marekani, Donald Trump

 

Matamshi hayo ya mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani kwamba kapu la vikwazo vya Washington dhidi ya Tehran halina chochote kingine cha maana, ni kukiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba Washington imetumia nguvu zake zote dhidi ya Iran lakini imeshindwa kutimiza malengo yake ya kufanya mazungumzo na Tehran na kuilazimisha ikubali mapatano yanayotakiwa na White House. Trump na genge lake huko Marekani walikuwa na ndoto kwamba, kwa kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vya kiwango cha juu kabisa ambavyo havijawahi kuwekewa nchi yoyote ile mfano wake, kungeliilazimisha Tehran iipigie magoti Washington na kukubali masharti yoyote itakayowekewa. Hata hivyo, zaidi ya miaka miwili imepita tangu Trump aanze kutekeleza sisa hizo za kijinai, na hadi leo viongozi wa ngazi za juu wa Marekani wanaomba kufanya mazungumzo na Tehran lakini wanakataliwa. Tab'an ugaidi wa kiuchumi, kijeshi na kimatibabu unaofanywa na serikali ya Marekani unawaletea madhara wananchi wa kawaida nchini Iran, na historia haitoweza kusahau jinai hizo.  Sasa hivi Trump na serikali yake wanalaumiwa vikali na wapinzani wao kwa kushindwa kuilazimisha Iran ifanye mazungumzo na Marekani, kwa kukosa mkakati madhubuti wa kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuipotezea heshima Marekani na kwa kuwapoteza waitifaki wake wakuu yaani nchi za Ulaya ambazo sasa zimekuwa zikichukua misimamo ya wazi ya kupinga siasa za Washington za kujikumbizia kila kitu upande wake. Uzeofu wa zaidi ya miaka 40 iliyopita unaonesha kuwa, kamwe Iran haijawahi kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani, hivyo Trump alipaswa kulielewa hilo kama anavyolaumiwa na wapinzani wake ndani na nje ya Marekani.

Marekani yakiri kufeli vikwazo dhidi ya Iran

 

Ikumbukwe kuwa mara kwa mara Washington inatangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran ili kuficha kushindwa kutimia ndoto zake. Vikwazo vya karibuni kabisa ni vile vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Benki na taasisi 18 za kifedha za Iran. Vikwazo hivyo vilitangazwa tarehe 8 mwezi huu wa Oktoba kwa nia ya kutia matatizoni zaidi juhudi za Iran za kujidhaminia mahitaji yake ya kimsingi. Pamoja na hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitumia muqawama wa kiwango cha juu ili kuvivunja nguvu vikwazo vya kiwango cha juu visivyo vya kibinadamu vya Marekani. Matunda ya muqawama huo ni pamoja na kutengwa kimataifa Marekani na sasa hivi viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo wanakiri kwamba wamemaliza vikwazo vyao vyote na hakuna kikwazo cha maana kilichobakia cha kuweza kuilazimisha Tehran ikubali matakwa ya kibeberu ya Washington. 

Kwa upande wake, Philip Gordon, mmoja wa washauri wa serikali ya zamani ya Barack Obama huko Marekani anasema: Tunapoangalia mlolongo wa hatua zilizochukuliwa na serikali ya Trump tutagundua kuwa, Trump amecheza kamari iliyofeli kuhusu kuilazimisha Iran ifanye mazungumzo na Marekani kwa ajili ya kupatikana kile Trump alichodai ni makubaliano bora. Trump na wenzake walikuwa wakidhani kwamba kwa siasa zao hizo watashadidisha machafuko ndani ya Iran, lakini hakuna chochote kilichotokea, na siasa hizo za Trump zimefeli.

Tags