Oct 27, 2020 07:24 UTC
  • Erdogan: Bidhaa za Ufaransa zisusiwe... viongozi wa sasa wa Ulaya ni Manazi na Mafashisti

Wakati mtifuano wa kisiasa baina ya Ufaransa na Uturuki ukiwa unaendelea baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kutoa matamshi ya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu na Waislamu, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametoa mwito wa kususiwa bidhaa za Ufaransa.

Erdogan, ambaye alikuwa akihutubia jana usiku kwa mnasaba wa kuanza maadhimisho ya "Wiki ya Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW", alimshambulia tena Rais wa Ufaransa kwa kumuelezea kuwa ni mtu mgonjwa na akabainisha kwamba, kushambuliwa Uislamu na Waislamu kulianza kwa uhamasishaji uliofanywa na kiongozi wa Ufaransa, ambaye yeye mwenyewe anahitaji kutibiwa akili.

Rais wa Uturuki ameongeza kuwa, kuufanyia uadui Uislamu na Waislamu imegeuzwa kuwa sera inayoungwa mkono na viongozi wa baadhi ya nchi za Ulaya.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Erdogan amemshambulia pia Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwa kumuuliza: Uko wapi uhuru wa kuabudu mnaodai kuwa upo? Vipi mnaruhusu askari polisi zaidi ya 100 Ujerumani washambulie msikiti?

Kampeni ya kupiga vita Uislamu na kueneza chuki dhidi ya Waislamu barani Ulaya  

Rais wa Uturuki ameeleza pia kuwa viongozi wa sasa wa Ulaya ni Manazi na Mafashisti na akasisitiza kwamba, watu wa Ulaya katu hawatopata chochote kwa uadui wanaoufanyia Uislamu.

Baada ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kutoa mwito wa kususiwa bidhaa za Ufaransa, maafisa wa serikali ya Paris wamesema, kwa sasa nchi hiyo haifikirii kuchukua hatua yoyote dhidi ya Ankara.

Hivi karibuni, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitamka kwa jeuri kuwa nchi hiyo itaendelea kuchapisha katuni zinazomvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW, jambo ambalo limewaghadhibisha Waislamu.

Kitendo hicho cha Macron kimesababisha kutolewa miito katika nchi za Kiislamu na Kiarabu zitoe ya kuanzishwa kampeni ya kususia bidhaa za Ufaransa duniani kote.../

Tags