Oct 28, 2020 07:41 UTC
  • Radiamali ya kindumakuwili ya Ufaransa kufuatia malalamiko ya Waislamu duniani

Waislamu duniani kote wamekasirishwa na kushadidi vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa hasa cha kuchapishwa tena katuni zinazomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW. Hasira za Waislamu zimeongezeka maradufu baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kutetea vitendo hivyo vya chuki dhidi ya Uislamu kwa kisingizo cha uhuru wa maoni.

Katika kubainisha malalamiko yao, hivi sasa Waislamu duniani wameanzisha kampeni ya kususia bidhaa za Ufaransa. Kampeni hiyo ambayo imeanza kupata mafanikio imewatia wasiwasi mkubwa wakuu wa Ufaransa ambao sasa wanachukua maamuzi ya kihamaki kukabiliana na hali hiyo. Serikali ya Ufaransa imechukua msimamo wa kindumakuwili kuhusu kadhia hii.

Katika upande mmoja, wakuu wa Ufaransa wanatupilia mbali uwezekano wa makabilianao baina ya Ufaransa na ulimwengu wa Kiislamu na katika upande wa pili wanatoa vitisho kwa nchi za Kiislamu kama vile Uturuki kutokana na nchi hiyo kuchukua msimamo imara dhidi ya Rais Macron.

Etienne Le Harivel Balozi wa Ufaransa nchini Sweden ametupilia mbali uwezekano wa makabiliano ya nchi yake na ulimwengu wa Kiislamu kutokana na matamshi yaliyojaa chuki dhidi ya Uislamu ya Emmanuel Macron. Balozi huyo ameashiria kuwepo karibu Wafaransa Waislamu milioni nane na hivyo kuufanya Uislamu kuwa dini ya pili kwa ukubwa nchini humo.

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu

Mwanadiplomasia huyo ametoa kauli hiyo katika hali ambayo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametoa matamshi yasiyo na msingi na kudai kuwa eti Uislamu ni dini 'iliyo katika mgogoro' kote duniani. Aidha ameongeza kuwa, serikali yake itatekeleza sera kali zaidi za usekulari. 

Katika hotuba ya hivi karibuni, Macron alisisitiza kuwa, Ufaransa itaendelea kuchapisha katuni zinazomvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad SAW. Kufuatia matamshi hayo kumeanzishwa kampeni katika mitandao ya kijamii ya kususia bidhaa za Ufaransa ambayo inajulikana kama #BoycottFrenchProducts.

Mufti Mkuu wa Lebanon Sheikh Abdul Latif Derian amesema kutusiwa Mtume Mtukufu SAW nchini Ufaransa ni uhasama kwa Waislamu wote duniani. Ameongeza kuwa, uhuru wa maoni hauna maana ya kuvunjia heshima itikadi za watu wengine na kwa msingi huo ufahamu wa 'uhuru kamili' unapaswa kuangaliwa upya."

Wakati huo huo, takwimu zinaonyesha kuwa, idadi kubwa ya watu nchini Ufaransa na kote Ulaya inazidi kuvutiwa na Uislamu na hivyo kusilimu na hiyo ni moja ya sababu ambazo zimempelekea Macron abainishe chuki zake dhidi ya Uislamu. Lakini chuki hizo badala ya kuwapeleka Wafaransa wachukizwe na Uislamu zitawapalekea wapate hamu zaidi ya kuujua Uislamu halisi na Mtume Muhammad SAW.

Katika upande mwingine, serikali ya Ufaransa imeanza kutoa vitisho kwa wale wanaoikosoa kutokana na misimamo yake ya chuki dhidi ya Uislamu. 

Gérald Darmanin Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa ameionya Uturuki kutokana na kile ambacho amesema ni uingiliaji wa nchi hiyo katika masuala ya ndani ya Ufaransa.

Kampeni ya kususia bidhaa za Ufaransa

Siku kadhaa zilizopita, Balozi wa Ufaransa mjini Ankara alitakiwa na serikali ya Ufaransa arejee nyumbani kwa ajili ya mashauriano baada ya matamshi makali ya Rais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki dhidi ya Rais wa Ufaransa. Erdogan aliashiria kauli zenye chuki dhidi ya Uislamu za rais wa Ufaransa na kusema kuwa Macron anapaswa kupimwa akili.

Swali linaloulizwa hapa ni hili, je, ni vipi Ufaransa sasa inalalamika wakati yenyewe huwa inaingilia mambo ya ndani ya nchi zingine na mfano wa wazi ni safari ya hivi karibuni ya Macron nchini Lebanon ambapo aliingilia wazi wazi mambo ya ndani ya nchi hiyo?

Hakuna shaka kuwa chuki dhidi ya Uislamu na kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW si suala la ndani ya Ufaransa. Ni kwa sababu ya nukta hiyo ndio leo Ufaransa inalaaniwa na kukosolewa na Waislamu na nchi za Kiislamu duniani na sasa uchumi wake utakumbwa na matatizo zaidi kufuatia kuanzishwa kampeni kubwa ya kususia bidhaa zake.

Tags

Maoni