Oct 28, 2020 08:00 UTC
  • Trump atoa madai mapya ya kichekesho, asema Biden akishinda urais, China itaimiliki Marekani

Rais Donald Trump ambaye anagombea muhula wa pili wa urais nchini Marekani kupitia chama cha Republican ameibuka na madai mapya ya kichekesho, ambapo amesema iwapo mshindani wake Joe Biden, anayewania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Democrat ataibuka mshindi katika uchaguzi wa mwezi ujao, basi Marekani itakuwa milki ya China.

Trump ametoa madai hayo katika ujumbe wake alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter leo Jumatano na kuongeza kuwa: Joe Biden, mgombea wa chama cha Democratic ni mwanasiasa fisadi ambaye anataka kuzipeleka China nafasi za ajira za Marekani, huku familia yake ikifaidika na mamilioni ya dola.

Trump amedai kuwa, iwapo Biden ataibuka mshindi katika uchaguzi wa rais utakaofanyika wiki ijayo, basi huo utakuwa ushindi mkubwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China.

Katika ujumbe wake huo wa kipropaganda, mwanasiasa huyo anayeandamwa na kashfa za ufisadi wa kifedha na maadili wa Repubican amedai kuwa, "iwapo Biden atashinda, China itaimiliki Marekani."

Trump na Biden ana kwa ana

Huku uchaguzi wa Marekani wa Novemba 3 ukizidi kujongea, Trump na Biden wameshadidisha cheche za matusi, kushambuliana na kutuhumiana.

Uchunguzi wa maoni katika miezi ya hivi karibuni unaonyesha kuwa, Biden anaongoza kwa zaidi ya asilimia 7 mbele ya Trump. Usimamizi mbovu wa janga la corona, ufisadi wa kimaadili wa Trump na ukandamizaji wa maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi ni miongoni mwa sababu ambazo zimechangia kupungua kwa kiasi kikubwa umashuhuri wa rais huyo wa Marekani.

 

Tags

Maoni