Oct 30, 2020 02:31 UTC
  • Waislamu wa Ufaransa walaani shambulio la kigaidi lililotokea nchini humo

Baraza la Waislamu wa Ufaransa limelaani shambulio la kigaidi lililotokea nchini humo.

Mbali na kulaani shambulio lililotokea jana Alkhamisi ndani ya kanisa la  Notre Dame katika mji wa Nice kusini mashariki mwa nchi, baraza hilo limetangaza kuwa, ili kuonesha mshikamano na kushiriki kwenye msiba wa familia za wahanga wa shambulio hilo limetoa mwito wa kuwataka Waislamu wa nchi hiyo waakhirishe sherehe za maadhimisho ya Maulidi ya Mtume Muhammad SAW. Waislamu wa Ufaransa wamesisitiza kuwa shambulio hilo haliwakilishi imani wala thamani za Uislamu.

Eneo la tukio

Watu wasiopungua watatu waliuawa jana na wengine kadhaa walijeruhiwa waliposhambuliwa na mtu mwenye kisu ndani ya kanisa la Notre Dame lililopo katika mji wa Nice. Mshambuliaji huyo alitiwa nguvuni, na kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ufaransa amelezwa hospitali. Hadi sasa haijafahamika sababu zilizomchochea mtu huyo kufanya shambulio hilo.

Shambulio jengine la kigaidi lilitokea masaa mawili baada ya shambulio hilo katikka mji wa Avignon ambapo mshambuliaji aliwahiwa kupigwa risasi na kuuliwa na askari polisi.

Wanazuoni wa Kiislamu pamoja na nchi mbalimbali za Kiislamu zimetoa taarifa za kulaani mashambulio hayo ya jana.

Hayo yanajiri huku uhusiano wa Ufaransa na Ulimwengu wa Kiislamu ukiwa umeingia doa baada ya matamshi aliyotoa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ya kutetea vitendo vya kumtusi na kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW ndani ya nchi hiyo.../

 

 

 

Tags

Maoni