Oct 30, 2020 08:00 UTC
  • Silaha zaondolewa madaukani Marekani kabla ya uchaguzi wa Jumanne ijayo

Sambamba na karibia tarehe ya uchaguzi wa rais wa Marekani, kampuni ya maduka makubwa ya nchini humo, Walmart imeanza kuondoa silaha na zana za kivita kwenye orodha ya bidhaa za madula hayo.

Gazeti la Washington Post limeandika kuwa kampuni ya Walmart ambayo ni miongoni mwa mashirika yanayomiliki maduka makubwa zaidi nchini Marekani, kuanzia jana Alkhamisi iliondoa silaha na bunduki katika orodha ya bidhaa za maduka hayo kwa hofu ya kutokea machafuko ya ndani baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Novemba 3.

Msemaji wa kampuni ya Walmart, Kory Lundberg amesema kuwa, kufuatia machafuko ya ndani katika miaka ya karibuni kampuni imeamua kuondoa silaha kwenye orodha ya bidhaa zake kwa shabaha ya kulinda usalama wa wafanyakazi na wanunuzi wa silaha hizo.

Kwa sasa kampuni hiyo inauza silaha za moto katika karibu nusu ya maduka yake makubwa nchini Marekani (hypermarkets) yanayofikia 4,700. 

Jumanne iliyopita televisheni ya CNN ya Marekani iliripoti kuwa Wizara ya Usalama wa Ndani ya nchi hiyo inajitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na machafuko na uasi wa kijamii baada ya uchaguzi wa Jumanne ijayo. 

Awali ripoti zilisema kuwa, kuongezeka ununuzi wa silaha kwa kiwango cha kutisha nchini Marekani kumezidisha hofu na wasiwasi wa kuzuka machafuko baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

Hisia za kukabiliwa na hatari zimezidi kuongezeka miongoni mwa Wamarekani kutokana na yale yanayoweza kujiri nchini humo katika siku zijazo kwa sababu ya hofu na wasiwasi kwamba baadhi ya watu wanaweza kutumia silaha moto kulalamikia matokeo ya zoezi la upigaji kura katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo utakaofanyika Novemba 3.

Hii ni baada ya kukamatwa pia kijana aliyekuwa na umri wa miaka 19 anayedaiwa kula njama ya kumuua Joe Biden, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic.

Ripoti za vyombo vya habari kuhusiana na hali hiyo zinatolewa wakati makundi wa wazungu wabaguzi wa rangi wanajiona bora yamejizatiti vikali kwa aina mbali mbali za silaha moto.

Mengi ya makundi hayo yanamuunga mkono Rais wa Marekani Donald Trump na yameshaonya kuwa yatachukua hatua endapo Trump atashindwa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais.

Maoni