Oct 30, 2020 08:54 UTC
  • Justin Trudeau
    Justin Trudeau

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amesema kuwa gaidi aliyetekeleza hujuma ya kigaidi katika mji wa Nice nchini Ufaransa hawakilishi dini ya Uislamu wala Waislamu, na kwamba watu wote wanapasa kukiri ukweli huo.

Trudeau amelaani hujuma hiyo katika mkutano wa Canada na nchi za Ulaya uliofanyika kupitia intaneti na kuitaja kuwa ni shambulizi la kigaidi.

Waziri Mkuu wa Canada amesema shambulizi hilo ni jinai mbaya na ya kidhalimu inayodunisha thamani za wanadamu wote, na anayetekeleza mashambulizi kama haya ni gaidi anayeua watu kwa damu baridi.

Hata hivyo Justin Trudeau amesisitiza kuwa, watu wa aina hii hawawakilishi dini ya Uislamu.

Matamshi haya ya Waziri Mkuu wa Canada yanatofautiana na yale yaliyotolewa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na serikali yake ambao wanang'ng'ana kuuhusisha ugaidi na dini ya Uislamu.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imetangaza kuwa mtu aliyefanya shambulizi la jana ndani ya Kanisa la Notre Dame katika mji wa Nice kusini mashariki mwa Ufaransa ni mkimbizi kutoka Tunisia aliyewasili nchini humo mwanzoni mwa mwezi huu kwa njia haramu akitokea katika kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.

Mtu huyo aliyeua watu watatu kwa kisu, amelazwa hospitali baada ya kujerihiwa vibaya kwa kupigwa risasi.

Kabla la shambulizi hilo la jana Alkhamisi, kulishuhudiwa visa kadhaa na hujuma zilizolenga Waislamu nchini Ufaransa likiwemo lile la kudungwa kisu wanawake wawili Wislamu wenye asili ya Algeria kandokando ya Mnara maarufu wa Eiffel mjini Paris.

Tukio hilo la wanawake wawili wazungu kuwadunga kisu wanawake hao Waislamu lilijiri Jumapili iliyopita lakini serikali na vyombo vya Ufaransa vilikataa kutoa taarifa yoyote kuhusu hujuma hiyo hadi juzi; suala ambalo limewakasirisha sana watetezi wa haki za binadamu na wadau wa mitandao ya kijamii.

Magazeti ya Ufaransa yamefichua kuwa, wanawake hao wawili wa Kiislamu walidungwa kisu wakati walipokuwa wakitembelea Mnara wa Eiffel wakiwa pamoja na watoto wao. Hujuma na mashambulizi hayo yaliambatana na matusi yanayowataka Waislamu kuondoka Ufaransa na kurejea katika nchi zao.

Tags

Maoni