Oct 30, 2020 12:39 UTC
  • John Ratcliffe
    John Ratcliffe

Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Ratcliffe amezungumzia tuhuma za Iran kuingilia uchaguzi wa mwaka huu wa Marekani ambazo sasa imebainika kuwa zimetolewa ili kuimarisha kampeni za uchaguzi za Donald Trump.

Jarida la Politico limeandika kuwa John Ratcliffe ametoa tuhuma hizo dhidi ya Iran bila ya kutegemea tathmini ya taasisi za usalama. Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari, wiki iliyopita Ratcliffe aliashiria baruapepe zinazodaiwa kutumwa eti na Iran na kudai kuwa, lengo kuu la baruapepe hizo ni kuwatisha wapiga kura, kuzusha machafuko ya kijamii na kutoa pigo kwa Rais Trump. Ajenda kuu ya mkutano huo wa John Ratcliffe na waandishi habari ilikuwa baruapepe hizo zinazodaiwa kutumwa kwa wapiga kura wa chama cha Democratic zikiwahimiza kumpatia kura zao Donald Trump. Matamshi ya kukinzana ya Ratcliffe yanaibua swali gumu kuwa, inawezekana vipi vitisho na hofu vinavyoelekezwa kwa wapiga kura wa chama cha Democratic vikiwataka wampigie kura Trump viwe na madhara na kutoa pigo kwa ya rais wa sasa wa Marekani? Na kwa namna gani taasisi za usalama za Marekani zimeshindwa kung'amua suala hili katika muda wa saa 24 baada ya kutumwa baruapepe hizo?

Madai hayo ya Ratcliffe kuhusu Iran yaliwashangaza maafisa wa taasisi nyingine za usalama za Marekani waliohudhuria mkutano huo wa waandishi habari. 

John Ratcliffe, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Marekani 

Hasa ikitiliwa maanani kuwa, madai ya Ratcliffe kwamba Iran imedhamiria kutoa pigo kwa Trump hayakutajwa katika taarifa yake kuhusu uingiliaji wa nchi za nje kwenye uchaguzi wa Marekani na ambayo ilisainiwa na Christopher Wray Mkurugenzi wa FBI na Christopher Carbs Mkurugenzi wa Taasisi ya Usalama wa Mitandao na Miundomsingi.  

Kwa utaratibu huo, imebainika kuwa Ratcliffe ,akiwa kama mkurugenzi wa taasisi ya Federali, si tu kwamba ameingilia kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani kwa kutumia cheo chake kwa maslahi ya mgombea mmoja yaani Rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump, bali kimsingi kadhia aliyoizungumzia yaani madai ya Iran kuingilia uchaguzi wa rais wa Marekani, imeibuliwa bila ya kushirikiana na wakurugenzi wengine wawili wa ngazi ya juu wa usalama na intelijinsia ambao walishiriki katika mkutano wake na waandishi wa habari. 

Hata hivyo hatua ya wakurugenzi hao wa ngazi ya juu ya kufichua kadhia hiyo ni sawa na kulalamikia hatua ya Ratcliffe ya kwenda kinyume na mamlaka yake ya kisheria; na ni dhahir shahir kwamba hatua hiyo ni kumfanyia Trump kampeni za wazi. Ratcliffe amedai kuwa Iran imefanya hujuma za kimtandao kwa lengo la kutoa pigo kwa Trump. Hii ni katika hali ambayo, katika kampeni zake za vyombo vya habari na mitandaoni, Tehran kimsingi inazingatia masuala na kadhia muhimu zinazoikabili jamii ya Marekani kama ubaguzi wa rangi, ukandamizaji mkubwa wa polisi, umaskini, kukosekana uadilifu baina ya matabaka ya watu, vitendo vya ubaguzi dhidi ya wahajiri, maandamano makubwa ya wananchi kulalamikia masaibu mbalimbali yanayowakabili na pia hatua na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za serikali ya Trump kama kujitoa katika makubaliano mbalimbali ya kimataifa na taathira zake hasi kwa uchumi na usalama wa dunia. Hata hivyo hatua hii, kwa mtazamo wa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wa Marekani, inakinzana na kampeni za uchaguzi za Trump. 

Rais Donald Trump wa Marekani   

Hii ni katika hali ambayo Washington ina rekodi ya muda mrefu sana katika kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine ikiwa ni pamoja na kuingilia masuala ya Iran; iwe kuingilia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika chaguzi mbalimbali duniani lengo likiwa ni  kufanya mapinduzi na kuziondoa madarakani serikali halali. 

Ali Bigdeli mchambuzi wa masuala ya Marekani anasema: Madai kwamba Iran inaingilia uchaguzi wa Marekani ni hatua ya kisiasa na yenye lengo la kuibua hisia za huruma katika jamii ya nchi hiyo kwa maslahi ya Trump. 

Viongozi wa ngazi ya juu wa Marekani wanadai kuwa nchi hasimu na zinazoipinga Marekani kama Russia, Iran na China zimeingilia mwenendo wa uchaguzi wa nchi hiyo katika hali ambayo kinyume kabisa na madai hayo, waitifaki wa Washington kama utawala ghasibu wa Israel unaotumia lobi za Kizayuni hususan AIPAC au utawala wa Saudi Arabia na waitifaki wengine wa Marekani ndio wanaoingilia uchaguzi wa rais wa nchi hiyo kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kwa kutoa misaada mbalimbali kwa kampeni za mgombea wanaomtaka na kuchukua msimamo dhidi ya mgombea wa upande wa pili kwa shabaha ya kudhamini maslahi yao. 

Lobi ya Uzayuni ya AIPAC  

Washington haipingi na inafumbia jicho uingiliaji kati kama, na mkabala wake maafisa wa taasisi za usalama na intelijinsia za Marekani wanazituhumu nchi hasimu na zinazoipinga sera za Washingon hasa nchi tatu yaani Russia, Iran na China. 

Tags

Maoni