Oct 31, 2020 02:38 UTC
  • Macron aendeleza vitendo vya kuuhujumu Uislamu; Trump aparamia mawimbi

Kushtadi vitendo vya chuki na hujuma dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa vinavyokwenda sambamba na uungaji mkono wa Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron kwa kisingizio kutetea uhuru wa kusema na kujieleza kumekabiliwa na radiamali mbalimbali na kuifanya nchi hiyo kubwa ya Ulaya ikabiiwe na wimbi kubwa la hasira.

Alkhamisi ya jana ilikuwa siku ya umwagaji damu huko Ufaransa. Katika tukio la awali lililojiri saa tatu asubuhi katika mji wa Nice, mtu mmoja aliyekuwa na kisu aliwashambulia watu kadhaa karibu na kanisa la Notre Dame la mji wa Nice ulioko kusini mwa Ufaransa. Kufuatia tukio hilo, polisi wa eneo hilo walithibitisha kuuliwa watu wasiopungua 3 na kujeruhiwa wengine kadhaa. Kabla ya mauaji hayo, vyombo vya habari vilitoa taarifa ya kupigwa risasi mtu mmoja aliyekuwa amejizatiti kwa silaha ya kisu katika mji wa Avignon kusini mashariki mwa Ufaransa na kisha kuuliwa mtu huyo. Alasiri ya Alhamisi ya jana pia polisi katika mji wa Lyon ilimkamata mtu mmoja aliyekuwa na silaha baridi ambaye ilisema alikuwa na nia ya kufanya shambulizi kwa kutumia kisu. Polisi ya Saudi Arabia pia imetangaza kuwa, imemtia mbaroni raia mmoja wa nchi hiyo ambaye alimshambulia mlinzi wa ubalozi mdogo wa Ufaransa mjini Jeddah.  

Silsila ya matukio yote hayo ya umwagaji damu ambayo ni jibu kwa vitendo vya chuki na uhasama vinavyoendelea kufanyika dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa yanaonyesha kuwa, mwenendo wa kuchukiza na usio wa kimantiki wa Emmanuel Macron wa kuunga mkono kwa pande zote hujuma na uhasama dhidi ya Uislamu ikiwemo hatua ya jarida la Charlie Hebdo ya kuendelea kuchapisha vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (S.A.W)  kwa kisingizio eti cha uhuru wa kusema hauna natija nyingine ghairi ya kuwachochea Waislamu na kuzidisha mivutano na makabiliano katika jamii ya Ufaransa. Kuendelea mwenendo huu wa sasa kutazidisha machafuko katika nchi hiyo ya Ulaya.   

Mara hii pia Rais Macron amelitaja shambulio la kisu katika mji wa Nice  kuwa ni "shambulizi la ugaidi wa Kiislamu" bila ya kuashiria nafasi yake kuu na misimamo yake dhidi ya dini ya Uislamu iliyochochea na kuhamasisha mashambulizi kama hayo. Amesema, Ufaransa haitasalimu amri mbele ya ugaidi katika kulinda thamani zake. Kwa hakika misimamo na mienendo hiyo ya Macron ya kudhihirisha chuki na kuhujumu Uislamu, kuunga mkono kuchapishwa vibonzo vinavyomvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu na vilevile uamuzi wake wa kuwasilisha muswada dhidi ya Uislamu, yote hayo yamezidisha mivutano na ukosefu wa usalama. Sayyid Hadi Burhani mchambuzi wa masuala ya Asia Magharibi anasema: Ufaransa ni moja kati ya nchi zenye huru mkubwa wa kukashifu na kutusi thamani za Kiislamu na kupiga vita dini hiyo. Suala hili yaani hujuma dhidi ya Uislamu na hujuma na mashambulizi dhidi ya hujuma hiyo vimeashiria pia na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Muhammad Javad Zarif katika ujumbe wake wa Twitter pale alipoandika kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali shambulizi la kigaidi lililotokea katika mji wa Nice nchini Ufaransa na kuongeza kuwa: Nafasi ya mzunguko huu batili wa kuzidisha uhasama, kueneza chuki, uchochezi na ukatili inapaswa kuchukuliwa na mantiki na utumiaji wa akili na busara. Dakta Zarif amesema: Pande zote zinapaswa kuelewa kuwa, uchupaji mipaka unafuatiwa na uchupaji mipaka zaidi, na haiwezekani kupatikana amani kwa vitendo au matamshi ya kichochezi.  
Hatua ya Emmanuel Macron ya kutumia "uhuru wa kujieleza na kusema" nchini Ufaransa kwa ajili ya kuhalalisha matusi na kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu imekosolewa sana hata ndani ya Ufaransa kwenyewe. Uvunjivu wa heshima na kutusi mambo matukufu ya kaumu au taifa fulani unatambuliwa kuwa ni kosa la jinai hata katika baadhi ya nchi zenye tawala za kisekulari zinazotenganisha baina ya dini ya siasa. 

Nukta nyingine muhimu katika matukio ya sasa nchini Ufaransa ni hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuparamia mawimbi. Trump anajulikana vyema kwa misimamo yake ya chuki na kupiga vita Uislamu na Waislamu. Kiongozi huyo wa Marekani amefanya jitihada za kufungamanisha ugaidi na Uislamu na ametumia matukio ya Alkhamisi iliyopita nchini Ufaransa kama kisingizio cha kunyoosha kidole cha tuhuma dhidi ya Waislamu na dini yao. Trump, kama alivyofanya mwenzake wa Ufaransa, Macron, ameyahusisha mashambulizi ya kigaidi ya Nice na dini ya Uislamu. Rais huyo wa Marekani ameandika kuwa: "Mashambulizi haya ya "ugaidi wa Kiislamu" yanapaswa kusitishwa mara moja, na si Ufaransa pekee bali hakuna nchi inayoweza kustahamili suala hili."

Misimamo hii inayofanana ya Trump na Macron na jitihada zao za kutaka kufungamanisha Uislamu na ugaidi vinafanyika kwa shabaha ya kutoa taswira isiyo sahihi na ya kupotosha kuhusiana na dini ya Mwenyezi Mungu, na vilevile kutengeneza kisingizio kipya cha kuzidisha mbinyo na mashinikizo dhidi ya Waislamu wanaoishi Ufaransa na Marekani.  

Tags

Maoni