Oct 31, 2020 10:01 UTC
  • Kusitishwa uanachama wa Corbny ndani ya chama cha Leba kutokana na misimamo yake dhidi ya Uzayuni

Jeremy Corbyn, kiongozi wa zamani wa chama cha Leba nchini Uingereza siku zote amekuwa akichukiwa na duru za Magharibi na Kizayuni kutokana na misimamo yake huru anayochukua hususan ya kupinga vitendo visivyo vya kibinadamu vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina kupitia matamshi na taarifa anazotoa.

Ripoti zinaeleza kuwa Jeremy Corbyn hivi sasa ametuhumiwa kupinga Uyahudi kutokana na misimamo yake aliyokuwa akidhihirisha wakati akiwa mkuu wa chama cha Leba; na hivyo amesimamishwa uanachama wake ndani ya chama hicho. Keir Starmer mkuu wa hivi sasa wa chama cha Leba nchini Uingereza juzi Alkhamisi alitangaza taarifa hiyo ya kusimamishwa uanachama Jeremy Corbyn mkuu wa zamani wa chama hicho kwa kile kilichotajwa kuwa ni hatua yake ya kupinga Uyahudi. 

Keir Starmer, Mkuu wa chama cha Leba nchini Uingereza 

Corbyn ambaye mara nyingi alikuwa akikabiliwa na mashinikizo katika duru za kisiasa za London kutokana na yeye kukosoa mara kwa mara jinai na ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina hivi karibuni amepinga ripoti ya Kamisheni ya Uadilifu na Haki za Binadamu ya Uingereza (EHRC) ambayo ndani yake ilidai kuwa, suala la kupinga Uyahudi lilikuwa jambo la kawaida wakati wa uongozi wake ndani ya chama hicho; na kueleza kama ninavyomnukuu: "vyombo vya habari na mahasimu wangu wa kisiasa wametia chumvi kupindukia kuhusu suala la kupinga Uyahudi katika chama cha Leba; na juhudi zangu za kufuatilia suala hilo hazijazaa matunda kutokana na ukwamishaji uliojaa urasimu wa chama cha Leba."  

Kusimamishwa uanachama Corbyn ambaye ni mmoja wa wanachama wa ngazi ya juu wa chama cha Leba kunaashiria mambo kadhaa. La kwanza ni kuwa, licha ya madai chapwa ya nchi za Magharibi ikiwemo Ungereza zinazodai kuwa zinaboresha uhuru wa kujieleza barani Ulaya na kujifakharisha na jambo hilo, lakini ukweli wa mambo ni kuwa uhuru huo ni kwa ajili tu ya masuala ambayo si mstari mwekundu kwa Wamagharibi; na nchi hizo hutoa radiamali na kupinga vikali kadhia zilizopigwa marufuku kama Holocaust pale zinapotiliwa shaka, kujadiliwa au kuchunguzwa na weledi na wachambuzi wa mambo. Aidha Nchi za Magharibi hutoa hukumu na vizuizi mbalimbali na kufikia kiasi cha kuwafunga jela watu hao wanaotilia shaka ngano kama ya Holocaust ya kuuliwa Mayahudi na Wanazi wa Ujerumani. Alireza Sultanshahi mchambuzi wa masuala ya Palestina anasema: Holacaust inatumiwa na Wazayuni kama wenzo na silaha ya kuhalalisha kila hatua na jinai zao katika kila pembe ya dunia; zikiwemo jinai zao katika ardhi za Palestina zinayokaliwa kwa mabavu na pia nje ya eno hilo. 

Kutilia shaka utambulisho na sura halisi ya utawala wa Kizayuni au kukosoa vikali jinai zinazofanywa na utawala huo haramu dhidi ya wananchi wa Palestina ni kati ya masuala yaliyopigwa marufuku katika ulimwengu wa Magharibi. Yaani sawa kabisa na alivyotuhumiwa Corbyn. Katika hali ambayo vitendo vya ukatili na visivyo vya kibinadamu vinavyofanywa kila uchao na Israel dhidi ya raia wa Palestina ikiwemo mzingiro wa muda mrefu uliowekwa na utawala huo haramu katika Ukanda wa Ghaza hadi mashambulizi ya anga na ya nchi kavu yanayofanywa mara kwa mara dhidi ya raia wa Palestina wakazi wa eneo, kuzikalia ardhi za Palestina na kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao za mababu na kwenye nyumba zao huko Baitul Muqaddas ya mashariki na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ambavyo vimegeuzwa na kuwa siasa endelevu na jambo la kawaida kwa utawala wa Kizayuni, havikubaliki na haviwezi kuhalalishwa hata kidogo. Binadamu yoyote aliye huru hawezi kunyamaza kimya na kukodolea macho tu jinai hizo dhidi ya Wapalestina. Jeremy Corbyn hivi sasa amekuwa mhanga mpya wa mashinikizo ya wafuasi wa utawala wa Kizayuni nchini Uingereza ambao hawezi kukabiliana na ukosoaji wowote wa Israel na jinai zake. 

Israel ikibomoa nyumba za raia wa Palestina huko Baitul Muqaddas  

Wakati huo huo Corbyn alikuwa akikosoa pakubwa na mara kwa mara mienendo na hatua za serikali ya kihafidhina ya Uingereza katika kuunga mkono waziwazi na kwa siri utawala wa Saudia katika kalibu ya kuiuzia Riyadh silaha za mabilioni ya dola, lengo likiwa ni kutekeleza mauaji dhidi ya wananchi madhlumu wa Yemen; alitaka kusitishwa uuzaji huo wa silaha kwa Saudi Arabia. Kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA pia Corbyn  alidhihirisha msimamo mkali na kupinga pakubwa hatua ya serikali ya Trump ya kujichukulia maamuzi kivyakevyake; na anaamini kuwa kujitoa Marekani katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018 ni chanzo cha matukio yaliyopelekea hali ngumu ya mambo inayoshuhudiwa  sasa. Hasa ikitiliwa maanani kuwa, Jeremy Corbyn alipinga vikali uingiliaji wa Donald Trump katika siasa za ndani ya Uingereza; na mara kadhaa ametahadharisha kuhusu malengo ya wabaya wake yaani kutekelezwa jitihada za kuifanya Marekani idhibiti uchumi na siasa za Uingereza katika kipindi baada ya Brexit. Suala hilo lilisababisha uhasama mkubwa kati ya Trump na Corbyn; na alishambuliwa kwa maneno mara kadhaa na Trump na kumtaja kuwa chaguo baya zaidi kwa ajili ya nafasi ya Waziri Mkuu wa Uingereza. 

Corbyn alipinga vikali hatua ya Marekani ya kujitoa ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA 

 

Tags

Maoni