Nov 16, 2020 02:33 UTC
  • Kukosolewa vikali madai ya kuwepo uhuru wa kujieleza nchini Ufaransa

Mwenendo wa chuki na kukejeliwa itikadi za Waislamu nchini Ufaransa umeshika kasi katika miaka ya karibuni, na katika uwanja huo kuchapishwa tena na jarida la Charlie Hebdo, vikatuni vinamvyodhalilisha Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) kumewakasirisha sana Waislamu.

Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, limetoa taarifa likikosoa madai ya kuwepo uhuru huko Ufaransa na kuituhumu nchi hiyo kuwa inatekeleza siasa za kinafiki na kundumakuwili na kusisitiza kuwa haistahiki kudai kwamba inaheshimu uhuru wa kujieleza. Shirika hilo limeashiria mifano kadhaa ya undumakuwili wa serikali ya Ufaransa ambapo limeashiria udhalilishaji uliofanywa hivi karibuni dhidi ya Mtume Mtukufu  (saw) na kusisitiza kuwa nchi hiyo haifai kudai kuwa inatetea uhuru wa kujieleza.

Moja ya mifano ya siasa za undumakuwili za Ufaransa ni kuhusu tukio la karibuni ambapo mwanafunzi mmoja wa Kichechnia alimuua mwalimu wake baada ya kukerwa na hatua yake ya kipumbavu na ya chuki ya kuonyesha darasani, vikatuni vya kumshalilisha Mtume (saw). Badala ya kukemea kitendo hicho na kujaribu kuwatuliza Waislamu waliokasirisha na dharau hiyo ya wazi dhidi ya matukufu yao, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliamua kuunga mkono kitendo hicho cha chuki dhidi ya Uislamu kilichofanywa na jarida la Charlie Hebdo, kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kusema. Haijulikani anakusudia nini hasa anapodai kuwa anatetea uhuru wa kusema. Je, kutusiwa na kukejeliwa matukufu ya dini ya Waislamu zaidi ya bilioni moja na nusu ulimwenguni ni alama ya kuwepo uhuru nchini Ufaransa? Kwa mujibu wa Sayyid Hadi Burhani, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi, Ufaransa ni moja ya nchi zilizo na uhuru mkubwa zaidi wa kutusiwa na kupigwa vita Uislamu na tahamani zake.

Emmanuel Macron mwenye chuki kali dhidi ya Uislamu na Waislamu

Katika kudumisha siasa zake za chuki dhidi ya Uslamu na Waislamu, hivi karibuni serikali ya Paris ilichukua hatua ya kufukuza idadi kubwa ya Waislamu na kufunga misikiti yao nchini humo. Ikiwa ni katika kudumisha hatua hizo hizo zisizo za kiutu dhidi ya Waislamu, polisi ya Ufaransa karibuni iliwakamata na kuwahoji kwa masaa kadhaa watoto wanne wa Kiislamu walio na umri wa chini ya miaka 10 ambao walikosoa kitendo cha mwalimu aliyeonyesha darasani vikatuni vya kumdhalilisha Mtume (saw).

Kwa matazamo wa Macron hakuna tatizo lolote katika kumtusi Mtume wa dini kubwa ya mbinguni lakini ni kosa na hatia kumtusi kiongozi wa serikali ya Ufaransa. Suala hilo lilidhihiri wazi mwaka 2019 ambapo watu wawili waliochoma kikaragosi cha Macron katika maandamano ya amani mjini Paris walikamatwa na kuhukumiwa kwa kosa la kumtusi kiongozi wa ngazi ya juu wa serikali. Isitoshe Macron mweneyewe sasa hivi anafanya juhudi za kupitishwa katika bunge la nchi hiyo sheria inayozuia kutusiwa na kufanyiwa kejeli katika mitandao ya kijamii, viongozi wa serikali.

Vilevile ni marufuku nchini humo kusaili na kuhoji madai ya kufanyika mauaji  dhidi ya Mayahudi mashuhuri kama holocaust au kukosolewa utawala wa Kizayuni, na wanaokiuka marufuku hiyo huadhibiwa mahakamani. Ufaransa pia imepitisha sheria kali zinazopiga marufuku wanawake wa Kiislamu kuvaa vazi la stara na kidini la hijabu katika baadhi ya sehemu zikiwemo shuleni na makazini.

Ufaransa inaruhusu Uislamu kutusiwa lakini inapiga marufuku kuhojiwa holocaust

Kwa msingi huo, ni wazi kuwa siasa na tabia za viongozi wa Ufaransa kuhusu Waislamu na Uislamu ni za kundumakuwili na madai ya kutetea uhuru wa kusema na kujieleza hutolewa tu pale Uislamu na matukufu yake yanapotusiwa na kuvunjiwa heshima. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, likasema: "Matamshi ya serikali ya Ufaransa kuhusu uhuru wa kujieleza, hayawezi kufunika unafiki wake wa kufedhehesha katika uwanja huo. Uhuru halisi hupata maana pale tu unaporuhusiwa kuwanufaisha wote katika jamii." Msimamo wa kiuhasama na kinafiki wa Macron dhidi ya Uislamu na uteteaji wake kwa wale wanaomdhalilisha Mtume Mtukufu (saw) na wakati huo huo kuutuhumu Uislamu kuwa ni sawa na ugaidi, ni njama inayotekelezwa kwa lengo la kuonyesha taswira isiyo sahihi kuhusu dini hii ya mbinguni na hivyo kupata kisingizio kipya cha kutoa mashinikizo dhidi ya Waislamu wanaoishi Ufaransa na vilevile kudumisha chuki na uonevu dhidi ya Waislamu.

Tags