Nov 17, 2020 07:30 UTC
  • Kukiri Obama kwamba jamii ya Marekani ina mpasuko na mgawanyiko wa kambi mbili

Mgogoro wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa, unaoendelea hivi sasa ndani ya Marekani, ambao umetokana na rais wa nchi hiyo Donald Trump aliyegombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican kukataa kwamba ameshindwa katika kinyang'anyiro hicho cha 2020 na Joe Biden aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Democratic, umepelekea kutolewa tahadhari na indhari kubwa juu ya hatari ya kugawanyika nchi hiyo.

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama ameiashiria nukta hiyo katika mahojiano aliyofanyiwa siku ya Jumapili na televisheni ya CBS alipoeleza kwamba, kupata kila mgombea urais katika uchaguzi wa Novemba 3 zaidi ya kura milioni 70 ni ishara kwamba Marekani iko kwenye hali ya mgawanyiko mkubwa.

Obama ameeleza pia kwamba, inavunja moyo kuona Warepublican wengi hawajafanya chochote kukabiliana na madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na Trump kwamba umefanyika udanganyifu mkubwa katika uchaguzi; na akaongeza kuwa: "Sisi hatuko juu ya kanuni. Sisi hatuko juu ya sheria. Hiki ndicho kiini cha demokrasia yetu."

Barack Obama

Kukiri Barack Obama kwamba kuna mpasuko na mgawanyiko mkubwa katika jamii ya Marekani kutokana na mgogoro wa kisiasa uliopo na kwamba jamii ya nchi hiyo imegawanyika katika kambi mbili za wafuasi wa Trump na wafuasi wa Biden, kunaonyesha kuwa Marekani inakabiliwa na mgogoro wa utambulisho na uwepo wake. Ukweli ni kwamba, tangu Donald Trump alipoingia madarakani Januari 2017 hadi sasa, na kwa kutilia maanani sera na hatua alizochukua, imejitokeza mielekeo miwili inayopingana kikamilifu katika muundo wa kiutawala na ndani ya jamii ya Marekani pamoja na hali mbili kinzani kuhusiana na sera na hatua hizo alizochukua Trump.

Trump, ambaye aliingia Ikulu ya White House akiwa ni mfanyabiashara asiye na rekodi ya utendaji katika uga wa siasa, alitekeleza sera zilizotafautiana kimuelekeo na za mtangulizi wake, yaani Barack Obama, na hivyo kuleta mageuzi makubwa ndani na nje ya Marekani yaliyokuwa na taathira mbalimbali. Kwa hivyo uchaguzi wa rais uliofanyika karibuni nchini Marekani baada ya miaka minne ya uongozi wa Trump, ulikuwa sawa na kura ya maoni ya kupima mtazamo wa jamii ya Marekani kuhusiana na sera na hatua alizochukua Trump katika uongozi wake. Kwa mujibu wa takwimu, katika uchaguzi wa mwaka huu, Trump amepata zaidi ya kura milioni 73 na Biden amenyakua zaidi ya kura milioni 78 za wapigakura wa Marekani. Jambo hilo linaonyesha kuwa, hitilafu na mpasuko haupo kati ya Warepublican na Wademocrat katika ngazi za utawala pekee na hasa ndani ya bunge la Kongresi, lakini mgawanyiko huo umesambaa pia hata ndani ya jamii ya Marekani.

Nukta muhimu ya kuzingatiwa ni kwamba, nyufa za mpasuko ulioko ndani ya jamii ya Marekani hazikuanzia katika kipindi cha utawala wa Trump na wala hazitokani na sera alizofuata yeye tu, bali kwa muda mrefu Marekani imegawanyika kuanzia ngazi ya weledi wenye vipawa hadi upeo wa jamii nzima; na hivi sasa imesibiwa na aina tofauti za mipasuko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi. Katika upeo wa kisiasa, kuzidi kuwa na utata utaratibu wa uendeshaji nchi na kuongezeka makundi yenye satua na ushawishi katika muundo wa utawala wa Marekani, kumesababisha maslahi ya watu binafsi, ya makundi au mirengo kuwa na nafasi ya juu zaidi kuliko maslahi ya kitaifa; na kutokana na kushadidi mipasuko ya kijamii na kujitokeza anga ya kambi mbili ndani ya Marekani, hitilafu na tofauti zilizopo zimevuka kiwango cha kawaida na kugeuka kuwa vita vya kiidiolojia baina ya mrengo wa kulia wa kihafidhina na ule wa kushoto wenye muelekeo wa demokrasia ya kisoshalisti.

Jambo hili limetishia na kuhatarisha umoja na mshikamano wa kijamii. Na ndiyo maana jamii ya Marekani imegawanyika katika kambi mbili juu ya masuala kama mfumo wa kodi, mfumo wa bima kwa wote, sera za uhajiri na namna ya kukabiliana na vitisho vya nje; hali ambayo imeshadidi katika kipindi cha utawala wa Trump. Kwa upande wa kijamii pia Marekani inashuhudia mpasuko mkubwa wa ndani juu ya masuala kadhaa likiwemo la ubaguzi wa rangi, umiliki wa silaha, vitendo vya ukatili na aina mbalimbali za ubaguzi, upendeleo na uonevu. Jamii ya Marekani ingali imezongwa na tatizo kubwa la ubaguzi wa rangi sambamba na kushamiri harakati za makundi ya kibaguzi. Si hayo tu, kungali kuna mjadala mkubwa baina ya mitazamo miwili inayokinzana kuhusu masuala muhimu kadhaa kama uhuru wa kubeba silaha ambao una uhusiano wa moja kwa moja na usalama wa jamii.

Kwa upande wa kiuchumi pia, ufa wa kitabaka umepanuka zaidi katika miaka ya karibuni na kusababisha mpasuko mkubwa baina ya masikini na matajiri ndani ya Marekani. Ni kama alivyoeleza Seneta Bernie Sanders kwamba mabilionea watatu wa Kimarekani wanamiliki utajiri mkubwa zaidi ya utajiri wa asilimia 50 ya watu wa tabaka la chini katika jamii.

Kutokana na yote hayo, Marekani sasa inaelekea kwenye mkondo wa kuporomoka; na moja ya vielelezo vya hali hiyo ni kuongezeka mpasuko na mgawanyiko ndani ya jamii ya nchi hiyo. Ukurasa wa Twitter wa lugha ya Kiingereza wa tovuti ya habari ya ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei uliandika yafuatayo kuhusiana na kushindwa Trump katika uchaguzi wa rais: "Bila kujali matokeo, kitu kimoja kiko wazi kabisa, nacho ni kuporomoka kusio na shaka kisiasa, kiraia na kiakhlaqi kwa utawala wa Marekani.../

 

Tags