Nov 18, 2020 02:23 UTC
  • Hitilafu katika kambi ya Warepublican kuhusu kuondolewa askari wa Marekani Asia Magharibi

Uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuondolewa askari wa nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi hususan Afghanistan na Iraq ambao unatarajiwa kutangazwa katika siku za usoni na iliyokuwa moja ya ahadi muhimu za Trump umekabiliwa na upinzani mkali wa chama chake cha Repulican katika Kongresi ya nchi hiyo.

Mitchell McConnell, kiongozi wa Warepulican katika Baraza la Seneti la Marekani ametangaza wazi upinzani wake kwa hatua ya kutaka kuondolewa askari wa nchi hiyo kutoka katika eneo la Asia Magharibi. Akizungumza katika kikao cha Seneti, McConnel amesema: Kuondoka kwa askari wa Marekani nchini Iraq na Afghanistan kutatudhoofisha na kuwaimarisha maadui zetu katika eneo la Asia Magharibi. Sisi tuna mchango mkubwa katika kulinda usalama wa taifa mbele ya magaidi. Wanachotaka magaidi ni kuondoka katika eneo hilo,  jeshi lenye nguvu kubwa zaidi duniani.

Msimamo wa wazi wa Mitchell McConnel, kiongozi wa Warepulican katika Baraza la Seneti la Marekani umetolewa baada ya kuenea habari kwamba, Trump anakusudia kupunguza idadi ya askari wa nchi hiyo walioko Iraq na Afghanistan kufikia Januari mwaka ujao wa 2021. Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentangon imetoa taarifa muhimu iliyoipa jina la ‘Agizo la Tahadhari’ kwa makamanda wa Marekani ambapo kwa mujibu wa agizo hilo imewataka makamanda hao kuandaa mipango ya lazima kwa minajili ya kupunguza idadi ya askari wa nchi hiyo huko Iraq na Afghanistan.

Rais Donald Trump akiwahutubia wanajeshi alipotembelea kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq

 

Pentagon inakusudia kupunguza askari 2,500 katika kila nchi yaani Iraq na Afghanistan. Filihali Marekani ina wanajeshi 4,500 nchini Afghanistan na wanajeshi 3,000 huko Iraq. Kabla ya hapo, Trump alikuwa ameahidi kwamba, hadi kufikia disemba 25 mwaka huu yaani wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi atakuwa amewaondoa na kuwarejesha nyumbani askari wote wa Marekani walioko katika mataifa ya Iraq na Afghanistan.

Hata hivyo jambo hilo lilikabiliwa na upinzani mkali wa Wizara ya Ulinzi Pentagon. Kutokana na upinzani huo, Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani akafutwa kazi kutokana na kuendelea kuonyesha waziwazi upinzani wake dhidi ya suala hilo. Baada ya Trump kumtimua Mark Esper alimteua Christopher Miller kukaimu nafasi hiyo. Watu ambao wameteuliwa na Miller kama washauri wake wanaipa nguvu dhana hii kwamba, Trump amemfuta kazi Mark Esper ili kuharakisha mchakato wa kuwaondoa wanajeshi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Wakati wa kufanyika mazungumzo baina ya Marekani na kundi la wanamgambo wa Taliban, Trump aliliahidi kundi hilo kwamba, atayaondoa majeshi yote ya nchi hiyo kutoka Afghanistan. Nukta muhimu ni hatua ya kundi la Taliban ya kupokea kwa mikono miwili ahadi hiyo na kuitaja kama hatua moja muhimu na chanya katika kutekeleza kivitendo makubaliano ya Qatar.

Wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan

 

Aidha Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq alifikia makubaliano na Donald Trump katika safari yake ya hivi karibuni mjini Washington kuhusiana na kupunguzwa idadi ya askari wa Marekani nchini Iraq.

Hivi sasa upinzani mkali wa kiongozi wa Warepublican katika Baraza la Seneti kwa uamuzi huu wa Trump unaonyesha kuwa, Warepublican wanatambua kuwa, uamuzi huu unalenga zaidi kupata himaya na uungaji mkono Trump kwa ajili ya kushiriki tena katika uchaguzi wa Rais mwaka 2024; ambapo kwa namna fulani utadhoofisha siasa za Washington mkabala na eneo la Asia Magharibi sambamba na kuzidi kuleta hali ya kutokuwa na imani waitifaki wa Washington kuhusiana na ahadi ya dola hilo la Kimagharibi katika uwanja wa kuwadhaminia usalama.

Hii ni katika hali ambayo, katika uga wa mamlaka nchini Marekani, kuna mtazamao mmoja baina vyama viwili hasimu vya Democrat na Republican kuhusiana na udharura wa kubakishwa askari wa nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi. Dana Stroul, mtaalamu wa Asia Magharibi anasema:  Ahadi ya Trump ya kuwaondoa wanajeshi wa Marekani huko Asia Magharibi haiendani sambamba na uhakika wa sasa wa uwepo wa wanajeshi wa nchi hiyo katika eneo hili.

Joe Biden, Rais mteule wa Marekani

 

Hii ni katika hali ambayo, Joe Biden, Rais mteule wa Marekani ambaye anatarajiwa kushika rasmi hatamu za uongozi wa Marekani Januari mwakani, anasisitizia kuendelea kubakia wanajeshi wa nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi na kutekelezwa uamuzi huu wa Trump wa kuondoa majeshi yote ya Washington katika eneo utakwamisha utekelezaji wa siasa za Rais mpya ajaye. Nukta muhimu ni hii kwamba, uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na Afghanistan haujawa na natija nyingine ghairi ya mauaji ya wananchi wa nchi hizo, uharibifu, hasara kubwa, kuongezeka ukosefu wa usalama na uzalishaji wa mihadarati na madawa ya kulevya ambao haujawahi kushuhudiwa.

Tags