Nov 18, 2020 10:33 UTC
  • Trump amfuta kazi afisa wa ngazi za juu aliyesema uchaguzi haukua na doa

Rais Donald Trump aliyebwagwa katika uchaguzi wa rais wa Marekani uliofanyika mapema mwezi huu amempiga kalamu nyekundu Mkurugenzi wa Wakala wa Usalama wa Mitandao na Miundomsingi wa nchi hiyo, kwa kutoa kauli iliyomghadhabisha kiongozi huyo kuhusu uchaguzi.

Trump anamtuhumu Christopher Krebs kuwa ametoa taarifa isiyo sahihi kwa umma, baada ya afisa huyo wa ngazi za juu wa Marekani kusema kuwa mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita haukuwa na dosari kama anavyodai mwanasiasa huyo wa Republican.

Katika siku za hivi karibuni, Krebs amekuwa akisisitiza kuwa, uchaguzi huo ulikuwa huru, sahihi na wa haki na kwamba madai ya kutokea uchakachuaji katika zoezi hilo hayana msingi wowote.

Mkurugenzi wa Wakala wa Usalama wa Mitandao na Miundomsingi wa Marekani ni miongoni mwa maafisa wa nchi hiyo wakiwemo hata wapambe wa Trump waliomkashifu rais huyo anayeondoka wa US, kwa madai yake ya kufanyika wizi katika uchaguzi, na kukwamisha mchakato wa kukabidhi madaraka.

Trump anasisitiza kuwa kura ziliibiwa kwa maslahi ya mshindani wake Biden

Hivi karibuni pia, Robert O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani alieleza kuwa, inaonekana kuwa Joe Biden ameshinda uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini Marekani.

Vyombo vya habari vya Marekani vilitangaza kuwa, Biden, mgombea wa kiti cha urais wa chama cha Democratic ameshinda uchaguzi wa rais wa nchi hiyo kwa kupata kura 290 za wajumbe wa Electoral College, mbali na kumpiga mweleka Trump katika kura za wananchi pia.

 

Tags