Nov 22, 2020 02:42 UTC
  • Juhudi za Trump za kutaka kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa Marekani

Hata baada ya kupita wiki mbili tokea ufanyike uchaguzi mkuu wa rais wa Marekani na matokeo yake kutangazwa, lakini bado Rais Donald Trump wa nchi hiyo anafanya juhudi kubwa za kubadilisha matokeo hayo.

Baada ya kuhesabiwa tena kura zilizopigwa katika jimbo la Georgia na kuthibitika tena ushindi wa Joe Biden mgombea wa chama cha Democrat, lakini bado Trump, mgombea wa chama cha Republican anashikilia msimamo wake hasi wa kutotambua ushindi wa Biden kama rais mpya wa Marekani. Gavana wa Georgia pamoja na waziri wake wa mambo ya nje wamethibitisha tena ushindi wa Biden baada ya kuhesabiwa kwa mara ya pili kura zilizopigwa katika jimbo hilo.

Nukta ya kushangaza hapa ni kuwa licha ya kuwa gavana huyo na waziri wake wa mambo ya nje ni wanachama wa chama cha Republican kama alivyo Trump mwenyewe, lakini rais huyo amekataa kabisa kutambua rasmi ushindi wa Biden, jambo linalothibitisha wazi kwamba yuko tayari kufanya lolote ikiwa ni pamoja na kuwapuuza wanachama wenzake wa Republivan, alimuradi aendelee kubakia katika ikulu ya White House kwa miaka mingine minne.

Hivi sasa kati ya majimbo tisa muhimu ya Marekani mabunge 8 ya majimbo hayo yanadhibitiwa na Warepublican. Kwa kutilia maanani kuwa ni wiki mbili tu zimebaki kabla ya kufanyika uchaguzi wa wanachama wa baraza la Electoral College hapo tarehe 14 Disemba, Trump anafanya juhudi za kupuuza uhalali wa uchaguzi wa hivi karibuni na hasa katika majimbo muhimu na kuwateua wajumbe wa baraza hilo kutoka miongoni mwa waungaji mkono wake ili aibuke mshindi katika mgogoro wa hivi sasa wa uchaguzi wa Marekani.

Wamarekani wakilalamikia mfumo wa Electoral College

Ni kutoka na ukweli huo ndipo Trump akawaalika hivi karibuni viongozi wa waliowengi katika bunge la Michigan huko White House ili wapate kuwashawishi wajumbe wa Electoral College katika jimbo hilo watoe uamuzi wao wa mwisho kinyume na matokeo ya kura katika jimbo hilo na hivyo kumpa Trump fursa ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo. Iwapo hilo litatimia, Biden atapoteza kura zote 16 za wanachama wa Electoral College wa jimbo hilo kwa manufaa ya Trump.

Trump pia anataka kutekeleza mbinu hiyo hiyo katika jimbo la Pennsylvania na majimbo mengine muhimu ya Marekani ili kumfanya Biden ashindwe kupata kura 270 za lazima za wanachama wa Electoral College na hatimaye kuwacha uamuazi wa nani atakayekuwa rais wa baadaye wa Marekani mikononi mwa bunge la Seneti la nchi hiyo. Katika hali hiyo uamuzi utaachiwa seneta mmoja tu kutoka kila jimbo, na hapo Trump ana matumaini makubwa ya kutangazwa mshindi kwa kutilia maanani kwamba ni Warepublican ndio walio na majimbo mengi kuwaliko Wademocrat.

Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Trump pamoja na timu yake ya wanasheria katika uwanja huo lakini hawajafanikiwa pakubwa na kufikia sasa kesi zote 28 walizoziwasilisha katika mahakama ya juu ya majimbo katika siku 18 zilizopita, zimetupiliwa mbali kwa kutokuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi wa hivi karibuni.

Kura za raia hazina umuhimu mkubwa katika mfumo wa uchaguzi wa Marerkani

Suala jingine ambalo limezua utata na ukosoaji mkubwa nchini Marekani kuhusu uchaguzi huo ni hatua ya chama tawala cha Republican kuendelea kumtetea Trump licha ya kushindwa wazi katika uchaguzi. Kwa hakika Warepublican wanakabiliwa na changamoto mbili muhimu. Ya kwa kwanza ni kuwa iwapo wataheshimu kura za wananchi ni Biden ndiye ataibuka mshindi na ya pili ni kwamba kama watapuuza suala hilo na kuamua kuwaunga mkono wafuasi sugu na wabaguzi wa rangi wa Trump ambao wanadai kuwa wizi ulifanyika katika uchaguzi, bila shaka watakuwa wameutilia shaka kubwa mfumo mzima wa uchaguzi wa Marekani.

Kwa kutilia maanani uungaji mkono wa kibubusa unaotolewa na wanachama wa Republican kwa Trump bila kuzingatia maslahi ya kitaifa, Benny Sanders, seneta huru wa nchi hiyo anasema kuwa chama cha Republican si chama cha kisiasa tena bali kimegeuka kuwa kundi la kidini na kiibada.

Tags