Nov 22, 2020 04:12 UTC
  • Sharti la kumfanya Trump akubali kuwa ameshindwa katika uchaguzi lawekwa hadharani

Mjumbe wa jopo la washauri wa rais wa Marekani ametangaza kuwa, Donald Trump atakubali ameshindwa katika uchaguzi wa rais endapo matokeo ya uchaguzi huo yataidhinishwa na Mahakama Kuu ya Serikali Kuu ya nchi hiyo.

Tovuti ya habari ya televisheni ya Sky News imemnukuu Gabriel Soma akieleza kwamba, endapo mahakama kuu ya Federali itatangaza kuwa hakuna udangayifu wowote uliofanyika wa kuweza kuathiri uwazi wa mchakato wa uchaguzi pamoja na matokeo yake, Trump atautambua na kuukubali ushindi wa Joe Biden, mshindani wake wa chama cha Democratic.

Soma ameongeza kuwa, "tunasubiri kuchunguzwa baadhi ya kesi tulizowasilisha katika mahakama za majimbo, ambako inavyoonekana kuna makosa yamefanyika kwa mtazamo wa sheria za uchaguzi."

Kwa mujibu wa mjumbe huyo wa jopo la washauri wa Trump, endapo mahakamu kuu ya shirikisho itamtangaza mshindi mgombea wa chama cha Democratic, Donald Trump ataheshimu uamuzi huo na mchakato wa kukabidhi madaraka utafanyika kwa kufuata utaratibu wake wa kawaida.

Hayo yanaelezwa katika hali ambayo, licha ya Joe Biden, mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic, kuongoza kwa kura za wananchi na za uwakilishi wa majimbo, Electoral College, hadi sasa Trump amekataa katakata kuyakubali matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Novemba 3 huku akikazania msimamo wake kwamba umefanyika udanganyifu mkubwa katika uchaguzi huo.../

Tags