Nov 22, 2020 06:52 UTC
  • IAEA yakiri kuruhusiwa kukagua maeneo inayoyataka ya nyuklia nchini Iran

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umetoa ripoti mpya na kuthibitisha kwamba umeruhusiwa kukagua maeneo ya nyuklia uliyoyataka nchini Iran.

Katika ripoti yake hiyo ya karibuni kabisa, wakala wa IAEA umethibitisha kuruhusiwa kukagua maeneo uliyoyataka ya nyuklia nchini Iran na kusisitiza kuwa, wakala huo unaendelea na shughuli zake za kuhakikisha miradi ya nyuklia ya Iran ni ya amani kikamilifu.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa katika vifungu 40, kwa mara nyingine imethibitisha kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitoa ushirikiano unaotakiwa kwa wakaguzi wa kimataifa wa nishati ya atomiki. 

Rafael Grossi

 

Licha ya wakala wenyewe wa IAEA kuthibitisha mara kwa mara ushirikiano mkubwa unaotolewa na Iran kwa wakala huo, lakini siku ya Jumatano, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa mara nyingine alikubali kuathiriwa na mashinikizo ya nchi za Magharibi na alidai kwamba anataka uwazi zaidi katika shughuli za nyuklia za Iran.

Grossi alitoa matamshi hayo katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakala wa IAEA, mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu na baada ya kumalizika ziara ya Rafael Grossi hapa Tehran, zilitoa taarifa ya pamoja na kutangaza kwamba, Iran ilijitolea yenyewe tu kuruhusu wakaguzi wa IAEA kutembelea maeneo mengine mawili na kufanya uchunguzi wao kuhusu ukweli unaosisitizwa mara kwa mara na Tehran kwamba, miradi yake ya nyuklia ni ya kiraia na ni salama kikamilifu; haina malengo yoyote ya kijeshi na wala ya kutengeneza silaha za atomiki.