Nov 23, 2020 01:04 UTC
  • Kuendelea chuki za rais wa Ufaransa dhidi ya Uislamu

Ikiwa ni kuendeleza chuki zake dhidi ya Uislamu na Waislamu, rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, sasa ametoa muhula maalumu kwa viongozi wa makundi ya Kiislamu ya nchi hiyo kuhakikisha wanajivika utamaduni wa Magharibi hata katika mambo ambayo ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Serikali ya Macron imeandaa hati maalumu iliyoipa jina la "Thamani za Warepublican" na kuwataka Waislamu watangaze utiifu wao kwa vipengee vyote vya hati hiyo katika kipindi cha siku 15 tu zijazo.

Hati hiyo iliyopendekezwa na Macron inawabana kupindukia Waislamu nchini Ufaransa, kuanzia kuwafungia njia za masomo ya nyumbani hadi kupangiwa maimamu wa misikiti wasome vitu gani na waache kabisa kusoma vitu gani.

Hatua hiyo ya Emmanuel Macron na serikali yake imewakasirisha mno Waislamu kote ulimwenguni, ikiwemo Taasisi kuu ya kijamii ya Kiislamu nchini Marekani inayojulikana kwa kifupi kwa jina la CAIR ambayo imemshutumu Macron na serikali yake kwa kutoa “makataa” na muda maalumu kwa Waislamu wa nchi hiyo kuhakikisha wanaachana na mafundisho ya dini yao na kujivika utamaduni wa Magharibi.

Maandamano ya kuilaani Ufaransa kwa kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW

 

Kwa mujibu wa Middle East Eye, baada ya matamshi ya siku ya Jumatano ya Emanuel Macron kwa Baraza la Waislamu wa Ufaransa (CFCM) ambapo aliwapa Waislamu “makataa” na muda wa siku 15 kuhakikisha wanajivika utamaduni wa Magharibi, Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu (CAIR) limemshutumu vikali Macron na kulaani kitendo chake hicho. Limesema, serikali ya Ufaransa haina haki ya kuwalazimisha Waislamu au watu wengine wowote wa jamii za wachache, kuachana na imani zao na kufuata tamaduni ambazo ni kinyume na itikadi zao kama ambavyo haina haki pia ya kuwalazimisha Waislamu kufasiri mafundisho ya dini yao kwa mujibu wa anavyotaka yeye Macron.

Tamko la taasisi hiyo kubwa zaidi ya kijamii ya Kiislamu nchini Marekani (CAIR) vile vile limesema, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Ufaransa imetekeleza sheria nyingi za kuwadhibiti na kutoa adhabu kwa Waislamu kiasi kwamba hata kuvaa nguo za staha ya mwanamke wa Kiislamu yaani Hijab kumepigwa marufuku maskulini na makazini kwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi Waislamu wa taasisi za serikali.

Hii ni katika hali ambayo maandamano makubwa yanaendelea katika kona mbalimbali za dunia, kulaani msimamo wa kiuadui wa rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kuhusu dini tukufu ya Kiislamu. 

Awali kabisa, Macron alinukuliwa akisema kwamba eti dini tukufu ya Kiislamu iko kwenye mgogoro. Baada ya hapo alijitokeza hadharani na  kuunga mkono kitendo kiovu na cha kifidhuli cha jarida la nchi hiyo la Charlie Hebdo cha kuchapisha vikatuni vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW. Baadaye rais huyo wa Ufaransa alijifanya kulegeza msimamo na kudai amenukuliwa vibaya, baada ya kuona ghadhabu kubwa za ulimwengu wa Kiislamu.

Chuki dhidi ya Uislamu si uhuru

 

Hata hivyo, rais huyo wa Ufaransa mwenye chuki za kidini bado anaendelea kuonesha uadui wake kwa Uislamu na Waislamu kwa kurudia misimamo yake ya huko nyuma kama vile kudai kuwa ufichuli wa jarida la Charlie Hebdo eti ni uhuru wa kujieleza na sasa amezuka na hati mpya ya kuwalazimisha Waislamu wafuate dini yao vile anavyotaka yeye Macron na si kwa mujibu wa anavyotaka Mwenyezi Mungu.

Wachambuzi wa mambo akiwemo Sheikh Mkuu wa al Azhar huko Misri, Ahmed al Tayeb wanaamini kwamba, hatua hizo za kueneza chuki dhidi ya Uislamu zinachukuliwa na rais wa Ufaransa kutokana na kufeli kwake kisiasa na kiuchumi hasa wakati huu wa kukaribia uchaguzi mkuu nchini Ufaransa.

Mhadhiri mmoja wa chuko kikuu chini Ufaransa ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kijamii anasema: Emmanuel Macron na serikali yake wako katika mazingira magumu sana hivi sasa kutokana na kufeli kwao kisiasa, kiuchumi na kijamii huku uchaguzi wa rais wa mwaka 2022 ukizidi kukaribia. Sasa hivi Macron anazusha makelele haya na yale ili asije akazidiwa nguvu na watu wenye misimamo mikali wa mirengo ya kulia. Lengo kuu la makelele yote haya ya Macron ni kupigania kuchaguliwa tena mwaka 2022.

Tags