Nov 24, 2020 05:57 UTC
  • Umoja wa Mataifa waipongeza Iran kwa juhudi zake za kutatua kisiasa mgogoro wa Syria

Katika hali ambayo ulimwengu umeshughulishwa na mapambano dhidi ya virusi vya corona, diplomasia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingali inaendelea kwa ajili ya kuleta usalama na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).

Katika uwanja huo, Ali Asghar Khaji, msaidizi wa ngazi ya juu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala maalumu ya kisiasa, na Geir Pedersen, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria siku ya Jumamosi walikutana mjini Tehran kwa ajili ya kuchunguza na kutathmini matukio ya karibuni nchini Syria na kuendelea kuwezesha kufanyika vikao vya kamati ya katiba ya nchi hiyo.

Pedersen ambaye aliwasili mjini Tehran akitokea Moscow Russia kwa ajili ya kujadiliana na viongozi wa Iran kuhusu Syria, ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu kutokana na kujudi zake za kuunga mkono utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Syria. Vile vile pande mbili zimebadilishana mawazo kuhusu taratibu zilizochukuliwa karibuni kwa sihirikiano wa wanachama wa kamati ya katiba ya Syria kuhusu ajenda na nyakati za kufanyika vikao vijavyo vya kamati hiyo. Pande hizo pia zimejadili matukio ya karibuni ya mkoa wa Idlib na kueleza matumaini yao kwamba amani ya kudumu itapatikana katika mkoa huo kwa kutekelezwa mapatano yaliyopo.

Geir Pedersen (kushoto) alipokutana mjini Tehran na Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Mashauriano yanafanyika kati ya pande mbili hizo katika hali ambayo, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani hivi karibuni alifanya safari katika eneo kwa ajili ya kuvuruga hali ya mambo na kueneza fitina katika eneo hili tata. Uzoefu wa huko nyuma unathibitisha wazi kwamba siasa za Marekani zimepelekea Syria kuwa moja ya nukta zenye migogoro mikubwa zaidi na kituo muhimu cha makundi ya kigaidi katika eneo. Katika kukabiliana na hali hiyo hatari kwa usalama, Iran, Russia na Uturuki zilibuni mpango wa kisiasa kupitia mazungumzo ya Astana na hivyo kuvunja siasa za Marekani za kutaka kuigawa Syria katika maeneo tofauti ya utawala na udhibiti.

Katika kutathmini umuhimu wa suala hilo, Wafiq Ibrahim, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: 'Baada ya kupita muongo mmoja wa mapigano ya kijeshi ya moja kwa moja na vile vile kutumia ugaidi kwa lengo la kutaka kuiangusha serikali ya Syria, Wamarekani wamegundua kuwa mradi wao nchini Syria umepata pigo kubwa ambalo limeulemaza kabisa.'

Matunda muhimu zaidi yaliyopatikana katika mazunguzo ya Astana ni kutatuliwa migogoro ya kieneo kwa njia za ndani ya maeneo hayo yenyewe. Umuhimu wa jambo hilo unaweza kutathminiwa kwa mitazamo miwili. Mtazamo wa kwanza ni kulindwa mshikamano wa kieneo kupitia ushirikiano wa pamoja kisiasa na kiusalama. Mtazamo wa pili ni kuzingatiwa na kusisitizwa umoja wa ardhi yote ya Syria.

Wanajeshi wa Marekani walioko Syria kwa ajili ya kupora mafuta ya nchi hiyo

Suala hilo lina umuhimu mkubwa na maalumu katika kutatuliwa mgogoro wa Syria. Matukio ya Syria hivi sasa yamepita marhala ya vita na kuingia katika hatua ya kutatuliwa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo, jambo ambalo bila shaka linaweza kuwa na mchango mkubwa katika kudhaminiwa uthabiti wa nchi hiyo kupitia katiba yake. Suala jingine muhimu katika uwanja huo ni kutiliwa maanani matatizo ya wakimbizi wa Syria katika mazingira magumu ya hivi sasa. Ni kwa msingi huo ndipo msaidizi wa ngazi ya juu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akasisitiza umuhimu wa kongamano la kimataifa la wakimbizi wa Syria lililofanyika hivi karibuni mjini Damascus, na wakati huo huo kuzikosoa nchi za Kiarabu ambazo hutoa nara tupu za kuwanga mkono wakimbizi wa nchi hiyo, kwa hatua yao ya kujaribu kuzuia kufanyika kongamano hilo muhimu. Hakuna shaka kuwa kurejeshwa usalama na utulivu wa kudumu nchini Syria ni kwa mslahi ya eneo zima la Asia Magharibi.

Kwa msingi huo, mashauriano kama hayo yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhalali wa kisiasa na kuandaa fursa nzuri kwa ajili ya kupatikana amani ya kudumu nchini Syria na katika eneo zima la Asia Magharibi.