Nov 24, 2020 07:16 UTC
  • Hatimaye Trump amekubali kumkabidhi madaraka Joe Biden

Baada ya kukataa kwa muda mrefu, hatimaye rais wa Marekani, Donald Trump amekubali kukabidhi madaraka kwa rais mteule wa nchi hiyo Joe Biden, suala ambalo linahesabiwa ni kukiri kushindwa Trump katika uchaguzi wa rais wa Novemba 3, 2020.

Mapema leo asubuhi, Donald Trump ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba amemtaka Emily Murphy, Mkuu wa Idara ya Huduma za Umma ya Marekani (GSA) achukue hatua zinazotakiwa kuhusu "protokoli za awali" kwa ajili ya kumkabidhi madaraka Joe Biden.

Kwa upande wake, Murphy amesema katika barua maalumu kwamba Joe Biden atafunguliwa milango ya kufikia vyanzo na huduma za Shirikisho ili kurahisisha zoezi la kukabidhiwa madaraka. 

Trump amelazimika kukubali kumkabidhi madaraka Biden baada ya maafisa wa uchaguzi wa jimbo la Michigan kudhibitisha kwamba Joe Biden amemshinda kwa kura nyingi Trump katika jimbo hilo.

Joe Biden

 

Kabla ya hapo pia Biden alishatangaza timu yake usalama wa taifa. Vile vile Biden jana alitangaza wajumbe muhimu wa serikali yake. Miongoni mwa wajumbe hao ni Antony Blinken ambaye ememteua rasmi kuchukuwa nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

John Kerry, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani wakati wa serikali ya Barack Obama, amepangiwa kuwa mjumbe maalumu wa serikali ya Biden katika masuala ya mazingira. 

Bi Linda Thomas-Greenfield ameteuliwa kuwa mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, na Jake Sullivan atakuwa mshauri wa usalama wa taifa katika serikali ya Biden.

Tags