Nov 24, 2020 13:24 UTC
  • Chanjo ya Corona ya China kugaiwa bure nchini Uturuki

Waziri wa Afya wa Uturuki amesema, dozi milioni kumi za chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 iliyotengenezwa na shirika la Sinovac la China itatolewa bila malipo kwa raia wa nchi hiyo.

Fakhruddin Kuja ameeleza leo kwamba, chanjo hiyo ya Covid-19 iliyotengenezwa China hivi sasa inafanyiwa majaribio kwa binadamu nchini Uturuki na inatolewa bila malipo kwa wote wanaojitolea kufanyiwa majaribio hayo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wanaojitolea wanaendelea kudungwa chanjo hiyo huku uchunguzi ukifanyika katika vituo 25 vilivyoko katika miji 12 ya Uturuki ili kubaini athari yake kwa kinga ya virusi vya corona. Watu 726 wa kada ya huduma za tiba na afya tayari wameshapatiwa chanjo hiyo, ambapo jumla ya watu wote waliodungwa chanjo hiyo ya corona hadi sasa ni 1,237.

Utengenezaji wa chanjo wa Covid-19 ya Sinovac

Waziri wa Afya wa Uturuki amesisitiza kuwa, taratibu zote za kisheria zinazohusu utumiaji wa chanjo hiyo zimekamilika na wafanyakazi wa sekta ya tiba nchini humo ndio wanaopewa kipaumbele cha kwanza cha kupatiwa chanjo hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Uturuki, baada ya watu wengine 153 kufariki dunia  nchini humo kwa ugonjwa wa Covid-19 katika muda wa saa 24 zilizopita, idadi ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa huo imeongezeka na kufikia 12,511…/