Nov 25, 2020 02:43 UTC
  • China yaishutumu “Marekani hatari” kwa kuzusha “fujo na machafuko” barani Asia

Ubalozi wa China nchini Ufilipino umelaani hatua za Marekani ulizozielezea kuwa ni za “kuzusha fujo na machafuko” katika bara la Asia

Ubalozi wa China mjini Manila umetoa tamko hilo baada ya mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani kutoa matamshi ya kuziunga mkono nchi zenye mzozo na China na kuituhumu Beijing kuwa inatumia mashinikizo ya kijeshi kufanikisha malengo na maslahi yake. Robert O’Brien alitoa matamshi hayo wakati wa safari yake ya hivi karibuni nchini Ufilipino.

Akiwa katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila juzi Jumatatu, O’Brien alisisitiza kuhusu msimamo wa Marekani wa kuendelea kutimiza ahadi zake kwa Taiwan na kuziunga mkono Ufilipino na Vietnam ambazo zina mgogoro na China wa masuala ya baharini.

Ubalozi wa China mjini Manila umeeleza katika taarifa kwamba, kauli hiyo ya O’brien ni ithbati kwamba lengo la safari ya afisa huyo wa Washington si kuunga mkono amani na uthabiti wa eneo la Asia bali lengo lake hasa ni kuchochea fujo na machafuko katika eneo hili ili kufanikisha maslahi ya ubinafsi ya Marekani.

Robert O'Brien

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya ubalozi wa China imesema: Marekani inapaswa iache kuchochea makabiliano katika Bahari ya China Kusini na vilevile isitishe utoaji matamshi yasiyo na nadhari na uwajibikaji kuhusu masuala ya Taiwan na Hong Kong ambayo ni mambo yanayoihusu China pekee.

Katika matamshi yake O’brien ameionya China kuwa endapo itajaribu kutumia vikosi vya jeshi lake ili kuishinikiza Taiwan itakabiliwa na matokeo mabaya.

Marekani na China zinatofautiana na kuvutana vikali juu ya kadhia kadhaa kuanzia teknolojia na haki za binadamu mpaka kuhusu hatua za kijeshi za China katika maji ya eneo lake na kila mmoja anamtuhumu mwenzake kuwa anafanya chokochoko na uchochezi wa makusudi.

Kwa upande wake, ubalozi wa China mjini Manila umeeleza kupitia taarifa yake kwamba, ukweli halisi wa mambo umethibitisha kuwa, Marekani ni mchochezi mkubwa kabisa wa kijeshi na ndiyo hatari kubwa zaidi kutoka nje ya eneo katika Bahari ya China Kusini…/