Nov 25, 2020 07:52 UTC
  • China yatoa onyo tena kwa Marekani kuhusiana na Taiwan

Kwa mara nyingine China imeionya Marekani kuhusiana na safari zinazofanywa na maafisa wa nchi hiyo katika kisiwa cha Taiwan.

Katika kauli aliyotoa kufuatia safari iliyofanywa na jenerali mwandamizi wa jeshi la wanamaji la Marekani huko Taiwan, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian ameionya Washington kwamba, hatua zake hizo cha kichochezi zina madhara kwa amani na uthabiti wa langobahari la Taiwan.

Lijian ameitaka Marekani ijaribu kudiriki unyeti ilionao Taiwan kwa Beijing na kuutambua msingi wa ardhi moja ya China inayojumuisha kisiwa hicho.

Licha ya malalamiko na upinzani wa serikali ya China, Michael Steadman, jenerali mwandamizi wa jeshi la wanamaji la Marekani alifanya safari hivi karibuni ya kuitembelea Taiwan.

Kabla ya Steadman, Waziri wa Afya wa Marekani Alex Azar na Keith Krach, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo waliitembelea Taiwan, kitendo ambacho kiliikasirisha serikali ya China.

China inaitambua Taiwan kama sehemu isiyotenganishika na ardhi yake na imeshaionya Marekani mara kadhaa kuhusu safari zinazofanywa na maafisa wa nchi hiyo huko Taipei pamoja na uuzaji wa silaha unaofanywa na Washington kwa kisiwa hicho na kuitaka iache kuwa na uhusiano nacho wa kijeshi wa aina yoyote.

Hivi karibuni, Marekani iliidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya dola bilioni moja na milioni 800 kwa Taiwan.

Katika kipindi cha miongo minne iliyopita Washington imekuwa ndiyo muuzaji mkubwa wa silaha kwa kisiwa hicho.../

Tags