Nov 26, 2020 14:56 UTC
  • Walimwengu waendelea kumuomboleza Maradona; Argentina yaanza siku tatu za maombolezo

Watu mashuhuri duniani na ulimwengu wa soka kwa ujumla, wanaendelea kuomboleza kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Argentina Diego Maradona, aliyefariki jana Jumatano akiwa na umri wa miaka 60.

Siku tatu za maombolezo ya kitaifa zimeanza nchini Argentina huku watu mashuhuri duniani wakiendelea kutuma salamu za rambirambi. Kulingana na msemaji wake, Maradona alifariki dunia kutokana na mshutuko wa moyo, ikiwa ni wiki mbili tu baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini alikofanyiwa upasuaji. Mchezaji huyo aliyeiongoza Argentina kutwaa kombe la dunia mwaka 1986, alifanyiwa upasuaji wa ubongo mapema mwezi huu. Maradona aliondoka hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa damu iliyokuwa imeganda katika ubongo wake, huku wakili wake Matias Moria akisema ulikuwa muujiza kwamba damu hiyo iliyoganda, ambayo ingesababisha kifo chake, ilikuwa imegundulika mapema.

Maradona, ambaye alichezea vilabu ikiwemo Barcelona ya Uhispania na Napoli ya Italia alikuwa nahodha wa timu ya Argentina na alishinda kombe la dunia mwaka 1986 na kufunga bao la kihistoria lililofahamika kama 'Hand of God'  Mkono wa Mungu dhidi ya Uingereza katika robo fainali.

Diego Maradona akinyanyua juu kombe la dunia baada ya kuiongoza nchi yake ya Argentina kulitwaa 1986

 

Katika mechi za Klabu Bingwa barani Ulaya zilizochezwa jana, watu wote uwanjani walikaa kimya kwa dakika moja kutoa heshima zao za mwisho, tukio ambalo linatarajiwa kutokea kabla ya kuanza kwa mechi zingine zote za Ulaya wiki hii.

Lionel Messi na Cristian Ronaldo ni miongoni mwa wachezaji waliotoa rambirambi zao, huku mchezaji wa Brazil Pele akisema alitarajia iko siku "wangecheza pamoja mpira".

"Kulikuwa na bango Argentina, mwaka mmoja uliopita, nililosoma ambalo lilikuwa limeandikwa: Haijalishi ulichokifanya katika maisha yako, Diego, muhimu ni kile ulichofanya katika maisha yetu,'" aliongeza Pep Guardiola mkufunzi wa Manchester City na aliyewahji kuwa kuwa kocha wa Barcelona na Bayern Munich.