Nov 27, 2020 02:30 UTC
  • Viongozi wa Ufaransa waendelea kutoa madai ya chuki dhidi ya Uislamu

Huku hasira za Waislamu kwa vitendo na matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa zikawa bado hazijapoa, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo ya bara Ulaya Jean-Yves Le Drian amejitokeza na kudai kwamba, baadhi ya mataifa yanataka kuwadhibiti Waislamu wa Ufaransa.

Jean-Yves Le Drian amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la al-Sharq al-Awsat na kudai kwamba, Ufaransa haina tatizo na Uislamu na Waislamu, lakini inachokipinga nchi hiyo ni juhudi za baadhi ya mataifa za kutaka kuwahodhi Waislamu wa Ufaransa.

Huku akikwepa kuashiria uungaji mkono wa nchi yake kwa makundi ya kigaidi nchini Iraq na Syria, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa amesema kuwa, nchi yake inakabiliwa na ugaidi mkubwa ambapo kwa upande mmoja inashuhudia harakati za makundi ya kigaidi kama Daesh na al-Qaeda na kwa upande wa pili inashuhudia mashambulio ya kigaidi ya mtu binafsi.

Maandamano ya kupinga matamshi ya rais wa Ufaransa dhidi ya Uislamu

 

Jean-Yves Le Drian amedai pia kuwa, kuna baadhi ya mataifa ambayo yana hamu na shauku ya kuwa na ushawishi wa kisiasa nchini Ufaransa na kuwadhibiti baadhi ya Waislamu.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni gazeti la Charlie Hebdo la nchini Ufaransa lilichapisha tena vikatuni vinavyomvunjia heshima Bwana Mtume SAW ambapo Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo ajitokeza hadharani na kulikingia kifua jarida hilo akidai kwamba, serikali yake inatetea uhuru wa kutoa maoni.

Hatua ya Rais Macron ya kuunga mkono kitendo cha kifidhuli cha jarida hilo imelaaniwa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu, huku kampeni ya kususia bidhaa za Ufaransa katika mataifa hayo ya Kiislamu ikishika kasi.

Tags