Nov 27, 2020 06:58 UTC
  • Bunge la Ulaya lapasisha kuwekewa vikwazo Uturuki

Wabunge wa Bunge la Ulaya jana walipasisha azimio la kuiwekewa vikwazo Uturuki kutokana na hatua zake katika eneo la mashariki mwa Barahari ya Mediterranean.

Shirika la habari la Tasnim limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, azimio hilo hata hvyo halina ulazima wa kutekelezwa. Limepasishwa kwa kura 631 ya ndio mbele ya kura 3 tu za hapana. Azimio hilo limesisitiza kuwa, viongozi wa nchi za Ulaya wanapaswa kutekeleza kivitendo vikwazo vikali dhidi ya Uturuki kama njia ya kuonesha kutoridhishwa kwao na hatua zilizochukuliwa na nchi hiyo huko mashariki mwa Bahari ya Mediterranean.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Wabunge wa Bunge la Ulaya wamesema kuwa wamepasisha azimio hilo kwa mashinikizo ya Ufaransa.

Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji

 

Katika kipindi cha wiki za hivi karibuni, kumekuwa na mzozo mashariki mwa Bahari ya Mediterranean kutokana na hatua zilizochukuliwa na Uturuki za kuanza kuchimba na kutafuta nishati kwenye eneo hilo.

Ugiriki kwa kushirikiana na Ufaransa na baadhi ya nchi za Ulaya zinadai kuwa, hatua hizo za Uturuki ni kinyume cha sheria na ni uchochezi. Nchi hizo ziliionya Ankara kuhusu madhara ya hatua zake hizo kwa Uturuki yenyewe.

Hata hivyo Uturuki imesema kuwa nchi hiyo haifanyi kitu chochote kilicho kinyume cha sheria, bali imechukua hatua hizo kwa mujibu wa sheria na ni sehemu ya haki yake katika Barahari ya Mediterranean.

Kiujumla kuna mzozo mkubwa baina ya Uturuki na Ugiriki hususan katika masuala ya vyanzo vya mafuta na gesi katika eneo la Mediterannean Mashariki.