Nov 28, 2020 04:43 UTC
  • Zakharova: Safari ya Pompeo katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu huko Syria ni upuuzaji wa sheria za kimataifa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameitaja safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu huko Syria kuwa ni ishara ya hatua za upuuzaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na Washington.

Akizungumza jana katika kikao cha kila wiki na vyombo vya habari, Maria Zakharova  amekosoa safari hiyo ya karibuni ya Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu huko Syria na kueleza kuwa Moscow inaitambua ziara hiyo kama ishara nyingine ya Marekani kupuuza sheria za kimataifa ili kukwamisha kupatiwa ufumbuzi migogoro ya Asia Magharibi. 

Zakharova ameongeza kuwa, jitihada za serikali ya Marekani kwa ajili ya kuhalalisha uwepo kinyume cha sheria Israel katika miinuko ya Golan huko Syria  ni kinyume na hatua ya Umoja wa Mataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la umoja huo. 

Katika hatua isiyo ya kawaida ambayo inakiuka sheria na maazimio yote ya Umoja wa Mataifa, tarehe 19 mwezi huu Pompeo alitembelea vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kisha akaelekea katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel huko Syria.

Mike Pompeo ziarani katika miinuko ya Golan, Syria  

Tags